TFF yawakingia kifua wanahabari
DAR ES SALAAM: Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limelaani tukio la kupigwa kwa mwanahabari baada ya kumalizika kwa fainali ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam FC uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Agosti 11 mwaka huu
Taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo yenye dhamana na mpira wa Tanzania imesema shirikisho hilo limeona picha inayotembea mitandaoni ikielezea Mwandishi wa Habari kudai kupigwa baada ya mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii.
“Kwanza, TFF inalaani kitendo hicho kwa vile mpira wa miguu si sehemu ya vitendo vya uvunjifu wa sheria, na tunaamini katika mchezo wa kiungwana ndani na nje ya uwanja.
Pili, tunafanyia kazi kubaini ukweli wa tukio hilo, na wote watakaobainika kwenda kinyume na taratibu za TFF katika usimamizi wa matukio yake watachukuliwa hatua kali” imesema taarifa hiyo
Taarifa hiyo imeenda mbali na kueleza kuwa “TFF inatambua umuhimu wa Waandishi wa Habari katika kukuza michezo, hivyo itaendelea kuwapa ushirikiano kuhakikisha wanafanya kazi yao vizuri na kwa weledi.”