
ZANZIBAR: TAMASHA la 23 la Kimataifa la Muziki, Sauti za busara linatarajiwa kuanza Februari 5 hadi 8, 2026 visiwani Zanzibar zikiwa siku nne za kuburudika na muziki wa live kutoka kwa wasanii zaidi ya 400 kutoka kote duniani.
Mkurugenzi wa Tamasha hilo Journey Ramadhani amesema kwa mwaka huu tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja tofauti na matamasha 22 yaliyopita ambayo yalifanyika katika Ukumbi wa Ngome Kongwe visiwani hapo.
Msanii mkongwe kutoka Mali Salif Keita ndiye ataongoza burudani katika tamasha hilo pamoja na wasanii wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwemo baadhi ya wasanii wa Tanzania, Ben Pol, Man Fongo, Alamokha na Man Kifimbo.
Licha ya burudani Tamasha hilo linatarajiwa kuinufaisha sekta ya utalii kupitia wageni wake ambao wengi wao ni watalii kutoka nchi mbalimbali wanaokuja kila mwaka kwa ajili ya tamasha hilo.




