
MOROCCO: Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Morocco, amesema mchezo wa leo dhidi ya Morocco utatoa mwanga wa nani anayepania kufuzu Kombe la Dunia.
Stars wanashuka dimbani leo saa 6:00 usiku katika jiji la Oujda, Morocco, wakipambana kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa fainali hizo.
Kocha Morocco ameeleza kuwa kikosi chake kipo katika hali nzuri, bila majeruhi, na wachezaji wote wako tayari kwa changamoto hiyo kubwa.
“Mechi hii ni kipimo kikubwa cha nani anayepania kufuzu. Nina imani na wachezaji wangu, hasa tunapocheza ugenini tunajitahidi kuwa wagumu na kupambana kwa ajili ya matokeo chanya,” amesema Morocco.
Pia amegusia hali ya hewa baridi inayoikabili timu tangu walipowasili Morocco, akisema awali ilikuwa changamoto kwa wachezaji, lakini sasa wameizoea na wako tayari kwa mchezo huo muhimu.
“Wachezaji wana morali kubwa na wanajua umuhimu wa mchezo huu kwa taifa letu. Tunapigania nafasi yetu kuelekea Kombe la Dunia, na kila mmoja anajua majukumu yake,” ameongeza.
Morocco tayari imeshajihakikishia nafasi nzuri ya kufuzuikiwa inaongoza kundi E na alkama 12, lakini kwa Tanzaniaambayo iko nafasi ya 3 ikiwa na alama 6 sawa na Niger wa nafasi ya pili, inahitaji ushindi au hata sare katika harakati za kufanikisha ndoto ya kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Macho na masikio ya Watanzania yapo kwa Taifa Stars, wakiwa na matumaini ya kuona kikosi chao kikionesha ubora na kupambana ili kusalia kwenye mbio za kufuzu.




