Ligi KuuNyumbani

Singida sahani moja na Simba, Yanga

BAADA ya raundi mbili kumalizika na Ligi Kuu Tanzania Bara kusimama kwa takribani wiki tatu kupisha timu ya taifa, Taifa Stars kucheza mechi za kimataifa, Simba wameendelea kung’ang’ania kileleni.

Pamoja na kuendelea kukalia kiti cha uongozi, Simba iko pointi sawa na watani zao Yanga na timu iliyopanda daraja ya Singida Big Stars kwa kila moja kuwa na pointi sita wakitofautiana uwiano wa mabao.

Simba msimu uliopita walishindwa kuonesha makali yao na kutowahi kukalia uongozi wa msimamo wa ligi hiyo licha ya kuwa mabingwa watetezi, msimu huu wameanza na moto.

Mabao matano ya kufunga, matatu katika mchezo wa kwanza dhidi ya Geita Gold na mawili katika mchezo wao wa pili dhidi ya Kagera Sugar wakifunga mabao 2-0 yamewafanya kutamba kileleni.

Yanga, mabingwa watetezi, nao wameanza kwa kasi baada ya kuzoa pointi zote sita katika michezo miwili, wakiwa katika nafasi ya pili baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania na 2-0 dhidi ya Coastal Union zote zikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid Arusha.

Singida Big Stars, timu iliyopanda daraja nayo imeanza kwa kasi baada ya kujikusanyia pointi sita hadi sasa baada ya mechi mbili wakishinda, 1-0 dhidi ya Prisons na 2-1 dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wao wa nyumbani, Liti mjini Singida.

Timu hiyo pamoja na ugeni wake katika ligi hiyo, baada ya mechi mbili imeng’ang’ania vigogo Simba na Yanga kwa kushika nafasi ya tatu.

Azam FC wameangukia katika nafasi ya sita baada ya juzi kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Geita na kuifanya Mtibwa Sugar kushika nafasi ya nne nao wakiwa na pointi nne pamoja na Namungo iliyopo katika nafasi ya tano.

Mbeya City walioanza msimu vizuri kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na kushika usukani, wameshindwa kuendeleza makali baada ya kufungwa na Singida Big Stars na kubaki na pointi zao tatu katika nafasi ya saba.

Timu nyingine zenye pointi tatu ni Ruvu Shooting, Tanzania Prisons na Coastal Union zikitofautiana uwiano wa mabao. Timu zenye pointi moja baada ya mechi mbili ni Polisi Tanzania, KMC na Geita Gold wakati timu ambazo hadi sasa hazina pointi hata moja ni Ihefu, Dodoma Jiji na Kagera Sugar.

Kwa upande wa wafungaji, Reliants Lusajo wa Namungo ndiye anaongoza katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu baada ya kufunga mabao matatu, huku Fiston Mayele wa Yanga na Moses Phiri wa Simba kila mmoja akizifumania nyavu mara mbili.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button