Ligi Daraja La Kwanza

SINGIDA FOUNTAIN GATE: Hakuna kulala CAF

TIMU ya Singida Fountain Gate Septemba 17 itakuwa na kibarua kigumu kuikabili timu ya Future ya Misri katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya Shirikisho la
Soka Afrika ikiwania kutinga hatua ya makundi.

Singida ambayo ni mara ya kwanza inashiriki michuano hiyo baada ya kupanda kushiriki Ligi Kuu msimu uliopita na kumaliza nafasi ya nne imefika hapo baada ya kuifunga JKU ya Zanzibar jumla ya mabao 4-3.

FUNZO LA JKU
Singida imekaribishwa vyema kwenye michuano hiyo na kuanza kupata funzo la mapema kabla ya kupiga hatua zaidi za mashindano hayo ya pili kwa umaarufu na ubora katika ngazi ya klabu Afrika.

Katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya awali, Singida ilipata ushindi wa mabao 4-1, waliporudiana JKU ilijitutumua na kupata ushindi wa mabao 2-0, hali ambayo ‘iliutetemesha’ uongozi wa Singida kwa namna moja ama nyingine.

Endapo JKU ingepata ushindi wa mabao 3-0, kibarua kingekuwa kigumu zaidi kwa Singida kupenya hatua inayofuata maana wangeanza kufikiria mikwaju ya penalti na kadhalika.
Hivyo kwa ushindani walioupata wa majirani zao hatua ya awali ni wazi wamepata mwanga wa hatua zinazofuata, ugumu na namna ya kutoridhika na matokeo ya mechi ya awali.

KOCHA MPYA
Ingawa Singida ni timu tishio tangu msimu uliopita katika michuano ya ndani lakini matokeo ya mechi dhidi ya JKU na mechi mbili za Ligi Kuu ambazo imetoka suluhu dhidi ya Tanzania Prisons na Tabora United, inaweza kuwa chanzo cha kuota nyasi kibarua cha kocha Hans Pluijm.

Timu hiyo imeongeza wachezaji wenye majina makubwa waliotua msimu huu kama Morice Chukwu, Maruf Tchakei, Duke Abuya, Beno Kakolanya, Dickson Ambundo, Thomas Ulimwengu walioungana na nyota wengine kama Meddie Kagere, Bruno Gomes lakini bado kikosi hicho kinaonekana kukosa muunganiko.

Kutua kwa kocha mpya, Ernst Middendorp raia wa Ujerumani kumeleta taswira mpya katika timu hiyo wakiamini ujuzi wake kupitia timu za St George, Kazier Chiefs, Chippa United, Moroka Swallows na nyingine unaweza kuwavusha hatua hiyo.

Mechi ya Future itakuwa ni kibarua chake cha kwanza kuonesha ubora na tija iliyomfanya
mabosi wa Singida wakampa nafasi katika benchi la ufundi la timu hiyo. Japokuwa presha ni kubwa kulingana na hadhi ya Singida katika michuano hiyo lakini ndoto ya mashabiki
wa timu hiyo kufanya vizuri dhidi ya Future imekuwa presha nyingine kwa Ernst.

PRESHA YA YANGA
Msimu uliopita katika michuano hiyo, Yanga ilitinga fainali na kufungwa kwa sheria ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa sare ya 2-2. Yanga ilifungwa nyumbani mabao 2-1 kabla ya kushinda bao 1-0 ugenini.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza Yanga kufanya hivyo na kuibua hamasa kwa klabu nyingi nchini kutaka kufanya kama hivyo, ambapo hata Singida licha ya ‘udogo’ wao katika mashindano hayo lakini wana ndoto hiyo pia!

Hivyo, hata kama Singida itafanya vibaya lakini sio kuondoshwa hatua hiyo na Future kwani wanahitaji kuweka rekodi ya kutinga hatua ya makundi kama ilivyo kaulimbiu ya kila timu kwa sasa kutoka Tanzania inayokwenda kushiriki michuano ya kimataifa.

Lakini Singida ikifanya hivyo itakuwa imeandika rekodi yake ya kutinga makundi katika msimu wao wa kwanza wa michuano hiyo, hivyo Ernst atakuwa amefanya jambo kwa timu
hiyo.

Kingine kinachoibua morali kubwa kwa timu za Tanzania kutaka kujitutumua vilivyo kimataifa ni hadhi ya Ligi Kuu Bara ambayo imetangazwa kuwa ni ya tano kwa ubora kwa sasa Afrika hivyo klabu nyingi zimepania kuonesha ubora huo kwa vitendo dhidi ya
timu nyingine Afrika.

FUTURE FC
Future ambayo awali ilikuwa ikifahamika kwa jina la Coca- Cola FC imeanzishwa miaka 12 iliyopita na huu ni msimu wa tatu inashiriki Ligi Kuu ya Misri. Katika msimu wa kwanza
ilimaliza katika nafasi ya tano kabla ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya nne na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Future inatajwa kuwa miongoni mwa timu tishio kwa sasa Misri licha ya umri mdogo ilionao ikielezwa imepania kumaliza utawala wa wakongwe Zamalek na Al Ahly kama ilivyo Pyramids ambayo nayo inafanya vizuri kwa sasa nchini humo na kimataifa.

Hivyo si timu nyepesi, si timu ya kubeza hata kidogo, ni timu iliyojipanga kwa ajili ya mapinduzi ya soka la Misri na Afrika pia kuelekea kulitangaza jina la timu yao mpya ambayo imekuwa ikishindana kwa usajili ghali dhidi ya Al Ahly, Zamalek na Pyramids.

Kwa kifupi Future ni kipimo sahihi kwa timu kama Singida inayohitaji kukua, kuleta mapinduzi na kujitangaza zaidi kutokana na uwekezaji na maono mapya waliyonayo, hivyo ni mechi iliyojaa ushindani na ndoto nyingi baina ya pande zote mbili.

Related Articles

Back to top button