
SOKA la vijana ni msingi wa maendeleo ya mpira kwa taifa lolote lililoendelea kimichezo duniani.
Kuna mataifa kama Nigeria, Ghana, Cameroon, Senegal, Brazil, Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, England na kwingineko yamefanikiwa kimichezo kutokana na uwekezaji katika soka la vijana.
Ukitazama klabu mbalimbali zenye majina makubwa duniani zina soka la vijana kuanzia umri mdogo wa chekechea, shule za msingi, sekondari ambapo zinawatafuta mataifa mbalimbali, zinawakuza, wanasoma na wengine wanakua na kuuzwa.
Klabu ya Ajax ya Uholanzi mwaka juzi ilitamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na asilimia kubwa ya wachezaji iliyokuwa nao ni wale iliyowaibua ambapo baada ya kutolewa wengi walinunuliwa kucheza soka la kulipwa Hispania, England, Ujerumani na kwingine.
Klabu kubwa zimekuwa zikifanya skauti ya kutafuta vijana kutoka katika vituo mbalimbali
kisha huwanunua kwenda kuwaendeleza vipaji vyao na huwatumia na wengine huuzwa klabu mbalimbali za Ulaya.
Vijana wanapokuzwa na klabu wale wenye vipaji wataitwa kwenye timu za taifa za vijana kwa mfano chini ya umri wa miaka 17 au 20 kushiriki mashindano mbalimbali yatakayowafanya waonekane na hatimaye kusajiliwa kwingine.
Imefika mahali klabu za Tanzania zinatakiwa zibadilike. Timu zinapoitwa kubwa basi majina yao na uwekezaji wao ufanane kwa kuleta kitu ambacho kitakuwa ni tofauti.
TANZANIA
Hapa Tanzania klabu ambazo zimekuwa zikijitahidi katika kukuza soka la vijana ni Azam FC, Mtibwa Sugar ambapo sio tu wanawachezesha bali wamekuwa wakiwapa nafasi ya kuonekana.
Pia, klabu kama Azam FC imekuwa ikiwapa nafasi vijana wake kwenda kucheza kwa mkopo kunako klabu nyingine zinazohitaji huduma zao lengo ni kuwatimizia ndoto kwa sababu na wao wanatamani kucheza, kuonekana na kufika mahali fulani.
Kwa mfano Azam FC iliwaibua baadhi kama Novatus Dismas kabla ya kwenda kwingine na baadaye kutimkia Ulaya. Kuna ambao walipita kama Simon Msuva, Morrice Abraham na
wengine.
Azam FC sio tu kwamba imekuwa ikizalisha vijana bali imekuwa ikifanya vizuri katika mashindano ya vijana kila mwaka kwa kumaliza nafasi za juu. Mtibwa unaweza kusema ni chuo cha kuzalisha vijana kwa muda mrefu na imewauza kunako klabu mbalimbali kama Simba, Yanga na kwingine na wanafanya vizuri.
Kwa kuwataja baadhi wanaoonekana kwa sasa kuna Kibwana Shomari, Dikson Job,
Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin na wengine wengi. Pia, timu hiyo bado imekuwa ikifanya
vizuri katika mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
Mtibwa Sugar iliandika rekodi ya kipekee kwenye soka la vijana U-20 kwa kufanikiwa kuwa timu ya kwanza kwenye michuano hiyo kuchukua taji hilo mara tatu mfululizo mwaka 2018, 2019 na 2021.
Na hata sasa bado wapo na walifuzu hatua ya robo fainali kuonesha kwamba wanaweza tena kufanya makubwa.
SIMBA
Ni miongoni mwa timu kongwe na kubwa nchini. Lakini ukubwa wake umeegemea katika mafanikio ya soka la wakubwa huku wakitumia nguvu nyingi kusajili wachezaji wa kimataifa kuendana na ushindani.
Simba miaka ya nyuma ilianzisha programu za kukuza vijana ambapo ilikuwa ikifanya skauti kisha inawalea na kuwapandisha. Wekundu hao walifanikiwa katika soka la vijana
kati ya miaka 2008 hadi 2015 wakati wakiwa wamemkabidhi Kocha Seleman Matola
majukumu ya kuwanoa vijana.
Matola alifanikiwa kuwaibua vijana 250 ambao baadhi walicheza Simba na wengine walikwenda kucheza klabu mbalimbali za Daraja la Kwanza ‘Championship’ na
Ligi Kuu.
Miongoni mwa wachezaji walioibuliwa wanaojulikana kwa sasa yumo Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na wengine ambao hakika waliitumikia vizuri Simba kabla ya kwenda
kucheza kwingine.
Baadaye Simba licha ya kuwa na timu za vijana kwa miaka ya karibuni walionekana wazi kutowapa kipaumbele vijana kwani hakukuwa na wachezaji wengine walioibuliwa labda
kipa Salim Juma ambaye amedumu mpaka sasa baada ya kulikalia benchi kwa muda mrefu.
Hata kama wapo huwapandisha kama ushahidi lakini hawapati nafasi ya kuonekana sana na baadaye huachana nao na kupandisha wengine ambao wanashindwa kuwasaidia.
Msimu huu timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Simba imefanya vibaya kwa kutolewa hatua ya makundi kwenye ligi yavijana wa umri huo.
Katika michezo mitatu iliyocheza haikushinda hata mmoja wala kufunga bao lolote. Ni aibu kuona timu kubwa kama Simba haiweki nguvu katika soka la vijana. Labda pengine msimu
ujao wakarudi kivingine baada ya kuamua kumrejesha kocha Matola kwenye soka la vijana. Hivi karibuni walimtangaza kuwa atakuwa sehemu ya viongozi watakaoibua vijana msimu ujao.
YANGA
Kama ilivyo kwa Simba, hata Yanga ni hivyo, kwani kwenye soka la vijana wako nyuma sana. Yanga ina timu za vijana na kuna wakati zinafanya vizuri na wakati mwingine ni hovyo.
Ukiacha msimu uliopita waliojitahidi labda na mwaka juzi. Lakini kuna vijana wanawapandisha kisha wanakalia benchi baadaye watasikika kwingine.
Kuna wachezaji vijana waliwahi kuvuma kama Omar Chibada, Gustavo Simon na Shaban Ramadhan waliwahi kupandishwa lakini hawakudumu kwenye kikosi hicho.
Msimu wa mwaka jana alipandishwa Clement Mzize ambaye angalau huyu alijitahidi kuonekana msimu huu baada ya kupewa nafasi na Kocha Nasreddine Nabi. Lakini uzalishaji wa vijana na kuwapa nafasi ya kuwaamini bado sio mzuri.
Kama wangekuwa wanapewa nafasi ya kuaminiwa na kutiwa moyo hakika wangekuwa wengi na wangewasaidia au pengine kuuzwa kwingineko. Pia, timu yake ya vijana chini ya umri wa miaka 20 msimu huu imeshindwa kufanya vizuri baada ya kutolewa hatua ya makundi.
Katika michezo mitatu imepoteza yote huku ikifunga mabao mawili na kufungwa matano.
Bado uwekezaji wa kweli unahitajika kwa timu hizo kuwa na timu bora za vijana zitakazoleta ushindani kwenye ligi ya ndani.
Kuwapa nafasi vijana ya kuonekana na kutimiza malengo yao. Ushindani wao
usionekane kwa timu kubwa, bali uanzie chini kuleta ladha ya mpira utakaoendana na majina na hadhi zao.