Africa

Simba yajiandaa kwa vita dhidi ya Al Masry

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameweka wazi kuwa anataka kuona kikosi chake kinapata mabao ya ugenini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry.

Simba, ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano hiyo ya CAF, wanatarajiwa kuondoka nchini Machi 28 kuelekea Misri kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Aprili 2.

Fadlu ameeleza kuwa Al Masry ni timu bora inayoshika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Misri, na hivyo ni wapinzani wenye uwezo mkubwa. Amesisitiza kuwa Simba italazimika kucheza kwa umakini mkubwa iwe na mpira au bila mpira.

“Tunapocheza ugenini, ni muhimu kufunga bao kwa sababu linasaidia sana katika mashindano haya. Tunakutana na changamoto kwa sababu tuna wachezaji vijana wasio na uzoefu wa hatua hii ya mashindano,” amesema Fadlu.

Akikumbuka enzi zake akiwa Orlando Pirates, anasema walikuwa wakicheza kila baada ya siku tatu, na iliwagharimu kwenye ligi baada ya kushindwa fainali.

Simba inakabiliwa na majukumu makubwa msimu huu, ikihitaji kushindania mataji matatu, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB, na kufika mbali kwenye michuano ya CAF.

“Wachezaji wanapaswa kuelewa umuhimu wao kwenye timu. hatupaswi kutegemea mtu mmoja, bali nguvu ya pamoja ndiyo itatufanikisha,” amesema Fadlu.

Timu hiyo sasa inajiandaa kwa safari yao ya Misri, huku lengo kuu likiwa ni kupata matokeo mazuri ugenini kabla ya mchezo wa marudiano nyumbani.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button