Nyumbani

Mchezo wa Simba na Dodoma Jiji Kuahirishwa

Tarehe Mpya Kutaangazwa

DAR ES SALAAM: BODI ya Ligi Kuu Tanzania TPLB imeuahirisha mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati Simba SC ya Dar es Salaam na Dodoma Jiji ya Dodoma ambao awali ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa KMC Complex Februari 15, 2025 kuanzia saa 10:00 alasiri.

Taarifa iliyotolewa na TPLB imeeleza sababu ya kuahirishwa kwa mchezo huo ni baadhi ya wachezaji na maofisa wa ufundi wa klabu ya Dodoma Jiji kutokuwa katika hali nzuri kiafya baada ya basi la klabu hiyo walilokuwa wakisafiria kutoka Ruangwa mkoani Lindi, kupata ajali majira ya saa tatu asubuhi katika Kijiji cha Matandu wilayani Kilwa mkoani humo.

Taarifa hiyo imeeleza zaidi kuwa ajali hiyo imesababisha athari hasi kwa klabu ya Dodoma Jiji kwa kuchelewesha safari yake ya kuelekea mkoani Dar es Salaam pamoja na kuathiri maandalizi ya kiufundi kwa kuwakosa wachezaji na maofisa wa ufundi ambao walipata majeraha.

Bodi ya Ligi Kuu imesema kuwa itatangaza tarehe mpya ya mchezo huo hivi karibuni.

Dodoma Jiji FC walipata ajali Februari 10, 2025 majira ya saa tatu asubuhi katika Kiji cha Matandu wilayani Kilwa mkoani Lindi wakati timu hiyo ilipokuwa ikisafiri kutoka wilayani Ruangwa kwenye mchezo wake na timu ya Namungo FC kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba Sports club ambao sasa utapangiwa tarehe nyingine.

 

Related Articles

Back to top button