Featured

Rogers: Tunaweza kupindua meza

PARIS, Kiungo wa Aston Villa Morgan Rogers amesema kikosi chao kina ubora na uwezo wa kupindua matokeo ya 3-1 waliyoyapata jijini Paris kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani ulaya hapo jana dhidi ya PSG watakapowakaribisha mabingwa hao wa LIgue 1 Villa Park.

Rogers ameiambia TNT Sports kuwa ni kweli ugumu upo lakini haipingiki kuwa Villa wanao uwezo na ubora wa kuiadhibu na kuiondosha PSG na anaamini nguvu ya mashabiki pia itakisaidia kikosi chake kilichotabiriwa kufanya makubwa UCL.

“Ni ngumu unapotakiwa kulinda na kushambulia kwa wakati mmoja, tulifanya hivyo lakini nahisi walikuwa bora nyumbani kwao au pengine makosa yetu. Ni lazima tuendelee na kuamini tunaweza, wala sina shaka ubora wetu unatosha kupindua matokeo, mechi haijaisha”

“Tunaenda nyumbani ambako tunapajua vizuri tunajua vizuri tunachezaje nyumbani, nyumbani huwa tuko bora kuliko sehemu yeyote ile”

Rogers ndiye ‘aliyechomoa betri’ dakika 35 ya mchezo wa jana kabla ya PSG kuwawashia moto na kupata mabao kupitia kwa Desire Doue, Khvicha Kvaratskhelia na Nuno Mendes na mchezo kumalizika 3-1.

Aston Villa walio katika nafasi ya 7 kwenye PL ‘watawatishia nyau’ PSG kwani huwa mwiba mchungu wawapo katika dimba hilo ambapo hawajapoteza mchezo tangu kipigo cha 2-1 mbele Crystal Palace kwenye kombe la Carabao mwezi October mwaka jana.

Related Articles

Back to top button