La Liga

RFEF yaufungia uwanja wa Sevilla

SEVILLE: SHIRIKISHO la Soka la Hispania (RFEF) limetangaza kuwa sehemu ya Uwanja wa Ramón Sánchez-Pizjuán nyumbani kwa klabu ya Sevilla itafungwa kwa mechi tatu zijazo baada ya mashabiki kurusha vitu uwanjani wakati wa kipigo chao cha mabao 2-0 dhidi ya Real Betis kwenye mchezo wa LaLiga Jumapili.

Kamati ya nidhamu pia imeitoza Sevilla faini ya euro 45,000 kutokana na tukio hilo, ambalo lilisababisha mchezo kusitishwa kwa dakika 15 baada ya vitu mbalimbali kurushwa kutoka nyuma ya goli la Fondo Norte.

Mwamuzi José Munuera alisimamisha mchezo na hatimaye kuwaongoza wachezaji kutoka uwanjani baada ya umati wa mashabiki waliokuwa katika eneo hilo kugoma kutii maelekezo ya kutulia.

Uwanja wa Ramón Sánchez-Pizjuán

“Sevilla FC itakata rufaa dhidi ya adhabu ya kufungwa kwa sehemu ya uwanja wa Sánchez-Pizjuán kutokana na matukio yaliyotokea wakati wa derby, tukifanya hivyo katika vyombo vya michezo na vile vya kawaida,” – klabu imesema katika taarifa.

Katika uamuzi wa ziada, kamati hiyo pia imemfungia mshambuliaji wa Sevilla Isaac Romero mechi mbili kwa kosa la kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na kitendo cha vurugu kilichotokea pembezoni mwa uwanja wakati wa mchezo huo huohuo. Klabu imesisitiza kuwa itapinga adhabu hiyo pia.

Sevilla ambao wanashika nafasi ya 13 wakiwa na pointi 16, wako nyuma ya Betis walioko nafasi ya tano na pointi 24.

Related Articles

Back to top button