Kwingineko

Reece James aonya joto kali Kombe la Dunia 2026

LONDON: BEKI wa England, Reece James, amesema wachezaji wanapaswa kujiandaa kwa mazingira magumu sana wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Amerika Kaskazini, kutokana na joto kali kipindi cha kiangazi.

James, aliyekuwa nahodha wa Chelsea katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu iliyofanyika nchini Marekani kati ya Juni 14 na Julai 13, alicheza katika hali ya joto kali mjini Philadelphia na dhoruba za mvua mjini Charlotte. Amesema hali hiyo imetoa funzo muhimu kwa kikosi cha England kuelekea Kombe la Dunia.

Mashindano hayo ya timu 48 yanatarajiwa kuwa na michezo 104 katika miji 16 ya Canada, Mexico na Marekani. Miji kama Dallas, Houston, Miami, Atlanta, Monterrey na Guadalajara inatarajiwa kuwa na joto la zaidi ya nyuzi 33°C katika miezi ya Juni na Julai.

“Wote tunafahamu hilo, na tunajiandaa kadri tuwezavyo. Ni mazingira magumu sana kucheza katika joto kama hilo, hasa kwa sisi tuliokulia England ambako hakuna hali kama hiyo,” – James aliwaambia waandishi wa habari.

Ameongeza kuwa kucheza mechi zenye muda wa kuanza usiku kutasaidia kupunguza athari za joto na unyevunyevu, huku akisisitiza umuhimu wa kukaa katika eneo moja ili kuzoea mazingira.

Hata hivyo, James, mwenye umri wa miaka 25, aliongeza kuwa ubora wa viwanja nchini Marekani haukuwa mzuri wakati wa Kombe la Dunia la Klabu, jambo lililoongeza changamoto.

“Viwanja tulivyochezea havikuwa bora, vilifanya mambo kuwa magumu zaidi, lakini tunatumai kufikia wakati wa Kombe la Dunia mambo yatakuwa yameboreshwa,” alisema.

England wanatarajiwa kuikaribisha Serbia leo Alhamisi kabla ya kusafiri kumenyana na Albania Jumapili, katika michezo yao ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia.

Related Articles

Back to top button