Afungwa maisha rushwa michezoni China

RAIS wa zamani wa Chama cha Mpira wa Miguu China(CFA), Chen Xuyuan, amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa hatia ya rushwa, Shirika la Habari Xinhua la China limesema.
Mwezi Januari, alikiri kupokea rushwa yenye thamani ya Yuan mil 81 sawa na shs bil 28.76.
Mahakama ya kati ya jiji la Huangshi katikati ya China imesema Chen alijihusisha na vitendo hivyo haramu toka mwaka 2010 hadi 2023, ambavyo vilijumuisha jukumu lake la awali akiwa Rais na mwenyekiti wa bandari ya Shanghai.
Waendesha mashitaka wamesema Chen alipokea fedha na vitu vya thamani kwa kubadilishana na kusaidia kupatikana mikataba ya miradi na kupanga matukio ya michezo.
Uamuzi wa mahakama hiyo umesema amesababisha uharibifu mkubwa kwenye sekta ya michezo ya China.
Kwa mujibu Xinhua pia maafisa wengine watatu wa mpira wa miguu wamehukumiwa kifungo cha kati ya miaka minane na 14 gerezani kwa kupatikana na hatia ya rushwa.