Rais Samia ampa pole Mzee Zorro

DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan amempa mkono wa pole Mwanamuziki mkongwe wa Muziki wa Dansi nchini, Zahir Ally Zorro.
Kwa niaba ya Rais Samia, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, jana alimtembelea mwanamuziki huyo kumjulia hali nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mwana FA amemkabidhi Mzee Zorro kiasi cha Shilingi milioni 10 taslimu kama salamu za pole na faraja kutoka kwa Rais Samia, akimtakia apone haraka.
Akizungumza baada ya kufika kumjulia hali, Mwana FA amesema Serikali inaendelea kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na wasanii wakongwe katika kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Tanzania na kuwa wasanii hao ni hazina muhimu ya taifa, hivyo wanastahili kuenziwa na kupewa faraja wanapokumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya au kijamii.
Kwa upande wake, Mzee Zorro alitoa shukrani zake kwa Rais Samia pamoja na Serikali kwa upendo na kujali hali yake, akisema msaada huo ni faraja kubwa kwake na kwa familia yake katika kipindi hiki anachopitia.




