Polisi waondoa video 154 za YouTube, reels 703 za wimbo ‘Tateeree’

HARYANA, India: POLISI wa jimbo la Haryana nchini India wameondoa jumla ya video 857 kutoka mitandao ya kijamii zinazohusiana na wimbo “Tateeree” wa msanii Badshah kufuatia kuzuka kwa utata kuhusu wimbo huo.
Wimbo huo umekosolewa vikali kwa madai ya kuwa na maneno na picha zisizofaa, hasa zinazodaiwa kudhalilisha wanawake na watoto.
Msanii huyo, anayejulikana pia kwa jina halisi Aditya Prateek Singh Sisodia, aliomba radhi na kuthibitisha kuwa wimbo huo umeondolewa katika majukwaa yote ya mtandaoni baada ya shinikizo kuongezeka.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka, video 154 zimeondolewa kutoka YouTube huku reels 703 zikifutwa kutoka Instagram. Hatua hiyo ilifuatia maagizo yaliyotolewa kwa kampuni za mitandao ya kijamii kuondoa toleo lolote la wimbo huo, ikiwemo nakala zilizopakiwa upya na vipande vifupi.
Mkurugenzi Mkuu wa Polisi Haryana, Ajay Singhal, alisisitiza kuwa maudhui yoyote yanayodhalilisha heshima ya wanawake na watoto hayatavumiliwa. Alionya kuwa akaunti zitakazohusika zinaweza kufungwa au kuzuiwa, huku wanaorudia makosa wakikabiliwa na hatua kali za kisheria.
Aidha, maafisa wameonya watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya kusambaza au kuunda maudhui yanayohusisha wimbo huo. Shibas Kabiraj naye aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka agizo hilo.
Kesi hiyo kwa sasa inachunguzwa baada ya kufunguliwa rasmi katika kituo cha polisi wa mtandao huko Panchkula, huku uchunguzi ukiendelea kuwabaini wote wanaohusika kusambaza maudhui hayo.
‘Tateeree’ ni wimbo wa hip hop wa Kiharyanvi uliotolewa Machi 1, 2026, ukiimbwa na Badshah kwa kushirikiana na mwimbaji Simran Jaglan. Mashairi yaliandikwa na Badshah, huku muziki ukitayarishwa na Hiten. Video rasmi ya wimbo huo iliongozwa na Mahi Sandhu na Joban Sandhu.
Wiki iliyopita, National Commission for Women ilimuita Badshah pamoja na watayarishaji wa wimbo huo kujibu tuhuma za maudhui machafu, ikisema kuwa wimbo huo unakiuka sheria mbalimbali za India zinazolinda heshima ya wanawake.




