Palmer nje wiki sita zaidi.

LONDON: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca, amesema kuwa mshambuliaji wa klabu hiyo Cole Palmer, atakosa michezo ya takriban wiki sita zijazo kutokana na majeraha ya goti yanayomsumbua, akiongeza kuwa hatua hiyo ni ya kuhakikisha anarejea akiwa katika hali ya utimamu.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa England hajaichezea Chelsea tangu walipofungwa na Manchester United Septemba 20 mwaka huu, wakati alipofanyiwa mabadiliko katikati ya kipindi cha kwanza kutokana na jeraha la goti lililokuwa likimtatiza tangu mwanzo wa msimu huu.
Maresca amesema alitumai Palmer angekuwa tayari baada ya mapumziko ya kimataifa yaliyotamatika hivi karibuni lakini sasa anasema hana uhakika kama mchezaji huyo tegemeo wa Chelsea atakuwa tayari hivi karibuni.
“Nilikosea kudhani angekuwa fiti kwa mchezo huu (dhidi ya Nottingham Forest). Lakini kwa bahati mbaya, atakuwa nje kwa wiki sita zaidi. Hii ndiyo taarifa mpya. Tunajaribu kumlinda Cole kadri inavyowezekana. Kitu cha muhimu zaidi ni kwamba atakaporejea, awe amekamilika kiafya na kimwili.” – amesema Maresca.
Aidha Kocha huyo aliongeza kuwa Palmer hatahitaji upasuaji, na akasema kuwa mujibu wa ratiba mpya, Palmer anaweza kukosa mechi sita au saba za Ligi Kuu, pamoja na michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na ya Kombe la Carabao dhidi ya Wolverhampton Oktoba 29.