Nyumbani

Oparesheni Berkane.

Simba yaziba pengo la mabao Zanzibar

ZANZIBAR:NAHODHA na beki tegemeo wa klabu ya Simba, Mohammed Hussein ‘Zimbwe JR’, amesema kikosi chao kina morali ya hali ya juu kuelekea mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco.

Mchezo huo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Jumapili, Mei 25, katika dimba la New Amaan Complex, Visiwani Zanzibar. Simba wanalazimika kushinda kwa mabao yasiyopungua 3-0 ili kufuta kichapo cha mabao 2-0 walichokipata katika mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Manispaa wa Berkane, Morocco.

Zimbwe JR ameeleza kuwa timu yao inaendelea na maandalizi makali kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, lengo likiwa ni kurekebisha makosa yaliyofanyika katika mechi ya awali.

“Hatma ya kombe iko mikononi mwetu wachezaji. Tuna morali kubwa sana na nguvu ya mashabiki kila kona, kwa sababu tuko nyumbani,” amesema nahodha huyo.

Ameongeza kuwa wanatambua umuhimu wa sapoti ya mashabiki wao, hasa kwa kuwa mchezo utafanyika nyumbani, ambapo kwa kawaida Simba hucheza kwa kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na ugenini.

“Wenzetu walipata matokeo mazuri nyumbani kwao kwa sababu ya sapoti kubwa, nasi pia tutakuwa na sapoti hiyo hiyo. Desturi yetu Simba tukiwa nyumbani huwa tofauti nina imani kombe hili linabaki nyumbani,” amesisitiza.

Simba sasa wanakabiliwa na mtihani mkubwa lakini wakiongozwa na morali, umoja na nguvu ya mashabiki wao, wana matumaini ya kufanya mabadiliko.

Related Articles

Back to top button