Tennis

Nyota wa Wimbledon, aomba milioni 1.4 kumwokoa Shangazi yake ICU

NAIROBI: MCHEZA tenisi nyota wa Kenya na mshindi wa taji la Wimbledon, Angella Okutoyi, amejitokeza kwa umma akiomba msaada wa milini 1.4 za Kenya ili kugharamia bili ya shangazi yake aliyelazwa katika chumba mahututi katika Hospitali ya Radiant jijini Nairobi.

Okutoyi, mwenye umri wa miaka 21, aliandika ujumbe wa kusikitisha akieleza hali ya shangazi yake:
“Taarifa kuhusu shangazi yangu, bado hali yake ni mahututi katika ICU ya Hospitali ya Radiant. Tunamshukuru Mungu kwa dalili ndogo za kuimarika, na tunaendelea kumtumainia kwa uponyaji wake. Bili imefika milioni 2 hadi sasa tumelipa Sh600,000 na tunahitaji Sh1.4 milioni. Mchango wowote utathaminiwa sana kwetu.” Alieleza.

Kisa cha shangazi yake kiliripotiwa awali na kuripoti kuwa anaugua Myasthenia Gravis, maradhi adimu ya kinga mwilini yanayosababisha misuli ya mwili kudhoofika na kuchoka kupita kiasi.

Wito wa msaada unatolewa chini ya saa 24 baada ya Okutoyi kupongezwa na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) kama Top Micro Youth Taxpayer (Youth Category) katika maadhimisho ya Siku ya Walipakodi, tarehe 20 Novemba.

KRA ilimsifu kuwa “mwenye kipaji, mwenye bidii na mzalendo,” ikitambua uadilifu wake wa kulipa ushuru.
Shangazi aliyemlea na Kumtia Nguvu
Shangazi yake, Cynthia Okutoyi, amekuwa nguzo muhimu katika safari ya Angella.
Katika mahojiano ya awali, Angella alimsifu shangazi yake akisema licha ya kuwa mgonjwa, hakuwahi kukosa kumtia moyo, ikiwemo kumfuata uwanjani wakati Kenya ilifanya historia kwenye Billie Jean King Cup.

Wiki iliyopita, Angella na mwenzake Francesca Pace walitwaa dhahabu kwenye michuano ya W35 Orlando women’s doubles, baada ya kuwashinda Wamarekani Maribella na Allura Zamarripa kwa seti 2–1.

Safari yake ya mafanikio ilianza kushika kasi mwaka 2022 alipoandika historia kuwa Mkenya wa kwanza kushinda taji la Grand Slam, akibeba ubingwa wa wasichana wa Wimbledon (doubles) akiungana na Rose Marie Nijkamp.

Mwaka 2023, alishinda dhahabu ya wanawake kwenye Michezo ya Afrika mjini Accra, na kuwa Mkenya wa kwanza kufanya hivyo baada ya miaka 46. Mshindi wa mwisho kufanikisha hilo alikuwa Jane Davies-Doxzon mwaka 1978.

Related Articles

Back to top button