Nikolas Jackson kupumzika wiki 8

BRIGHTON: Bosi wa Chelsea Enzo Maresca amethibitisha kuwa mshambuliaji wake raia wa Senegal Nicolas Jackson atakuwa nje ya uwanja mpaka baada ya mapumziko ya kupisha michezo ya kimataifa mwezi Machi kutokana na majereha ya misuli.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Alhamisi Maresca amesema walidhani jeraha la mshambuliaji huyo halitokuwa kubwa lakini sasa madaktari wanasema anahitaji muda wa kuwa sawa.
“Nico atakuwa nje mpaka baada ya mapumziko ya michezo ya kimataifa pengine zaidi ya hapo, nilidhani jeraha sio kubwa lakini sasa naona atakosekana kwa wiki sita au nane, sitaki kumshinikiza acheze. Nitasubiri awe sawa. ” amesema.
Maresca pia amesema mshambuliaji wake mwingine Marc Guiu nae hatakuwa sehemu ya kikosi hicho kutokana na jeraha kama hilo.
Hata hivyo Maresca alitangaza habari njema kumhusu kurejea hivi karibuni kwa kiungo Romeo Lavia na beki wa kati Benoit Badiashile huku Wesley Fofana akiwa amerejea mazoezini japo atahitaji wiki 2 mpaka 3 kuanza kucheza.