AFCON
Ndidi:Wasipolipa posho nitawalipa mimi

RABAT:NAHODHA wa Nigeria, Wilfred Ndidi, ameamua kubeba jukumu zito ndani ya timu ya taifa baada ya kutangaza kuwa yuko tayari kulipa mwenyewe bonasi za wachezaji na benchi la ufundi iwapo Shirikisho la Soka Nigeria (NFF) litashindwa kufanya hivyo kabla ya robo fainali ya AFCON dhidi ya Algeria.
Ndidi amesema tayari amekuwa akihamasisha kikosi kizima kuacha kujiingiza kwenye masuala ya nje na badala yake wajikite kwenye maandalizi ya mechi.
“Nimekuwa nikisukuma timu ifanye mazoezi na ijiandae tangu mchezo wa pili. Sasa nimewaahidi wachezaji na benchi la ufundi kwamba nitawalipa mwenyewe bonasi kama mamlaka zitashindwa kufanya hivyo kabla ya Jumamosi,” amesema Ndidi.
Nyota huyo ameweka wazi kuwa hataki kabisa suala la bonasi liingie kichwani mwa wachezaji na kuathiri maandalizi yao. “Sitaki hizi fedha zisizolipwa ziathiri maandalizi yetu,” ameongeza.
Hatua hiyo ya Ndidi imewavutia wengi, mashabiki wakimtaja kama nahodha wa kweli, aliyeamua kubeba jukumu ili kulinda umoja na morali ya timu kuelekea mechi kubwa dhidi ya Algeria.




