Ligi Kuu

Nasreddine Nabi, ashuhudia mechi ya Simba Vs Singida

DAR ES SALAAM: KOCHA wa klabu ya Kaizer Chiefs kutoka Afrika Kusini, Nasreddine Nabi na msaidizi wake Cedric Kaze walionekana katika uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam jana Mei 28, 2025 wakifuatilia kwa makini mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC na Singida Black Stars.

Nabi, ambaye aliwahi kuwa kocha mkuu wa klabu ya Yanga SC, alipata nafasi ya kushuhudia ushindi mwembamba wa bao 1-0 uliopatikana na Simba katika mchezo huo uliovutia mashabiki wengi.

Uwepo wake uwanjani umeibua maswali mengi miongoni mwa wadau wa soka, hasa ikizingatiwa kuwa hajakuwa akihusishwa na shughuli za soka la ndani kwa muda mrefu.

Taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika zinaeleza kuwa kocha huyo yupo nchini kwa lengo la kufanya mazungumzo na Feisal Salum ‘Fei Toto’, kiungo wa Azam FC, ambaye kwa sasa anahusishwa na tetesi za kuhitajika na klabu tatu kubwa  Kaizer Chiefs, Simba, na Yanga. Yanga, ambayo ni klabu yake ya zamani, inaripotiwa kuwa na nia ya kumrejesha kiungo huyo mahiri.

Ujio wa Nabi unaweza kuwa ni sehemu ya mipango ya Kaizer Chiefs kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu mpya, huku wakitafuta vipaji vya kuvutia kutoka Tanzania ambavyo vinaendelea kuonesha ubora katika ligi ya ndani.

Mashabiki wa soka wanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mazungumzo haya, huku wengi wakijiuliza iwapo Fei Toto ataondoka Azam FC, na iwapo atajiunga na timu ya zamani ya kocha wake wa zamani, Nasreddine Nabi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button