Muziki

Mwimbaji wa Injili kutoka Rwanda atua Tanzania kufanya tamasha

MWIMBAJI wa Nyimbo za Injili kutokea nchini Rwanda Israel Mboni anayetamba na wimbo wake wa ‘nina siri’ ametua nchini Tanzania tayari kutoa huduma katika tamasha la uimbaji.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Novemba 2 na 3 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City na viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Israel amesema anafurahi kuja nchini Tanzania kufanya huduma na anawapenda sana watanzania.

“Nimekuja kutoa huduma ya uimbaji, tutaimba na kucheza pamoja na watanzania na kufurahia wakati wa Mungu. Naamini watabarikiwa na kazi ya Mungu nitakayofanya, watu wajitokeze kwa wingi, rafiki zangu waje kufurahia matendo makuu ya Mungu.

Muandaaji wa ibada hiyo ya kumsifu Mungu Lilian Mkumbo amewataka watu kujitokeza kwenye ibada ya Wakati wa Mungu na kufurahia lakini pia amesema hadi sasa mwitikio ni mzuri, watanzania wamepokea kwa wingi.

Kwa upande wake Muimbaji wa nyimbo za Injili nchini Tanzania, Rehema Semfukwe amesema kuwa upendo walioonyesha watanzania ni mkubwa kuanzia kwenye mapokezi  katika uwanja wa ndege,kilichobaki ni kujitokeza kwenye tamasha.

“Usipange kukosa baraka hizi ni kubwa mno katika ibada, njooni tuimbe na kucheza kwa pamoja. Tuje kumshukuru Mungu, wote mnakaribishwa.

Msanii huyo atasindikizwa na wasanii mbali mbali kutoka nchini Tanzania wakiwemo Rehema Semfukwe, Paul Clement, Joel Lwaga, Boaz Danken, Upendo Nkone, Bella Kombo na wengine wengi.

Related Articles

Back to top button