MwanaFA ataka Stars ‘isapotiwe’ kwenye CHAN

DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ amewahimiza watanzania wote kuiunga mkono timu ya taifa itakayoshiriki michuano ya CHAN 2024, akisisitiza kuwa maandalizi muhimu tayari yamekamilika na sasa ni zamu ya wachezaji kuonesha uwezo wao uwanjani.
Kupitia ujumbe aliouweka leo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kushiriki hamasa ya CHAN 2024 iliyofanyika Mbagala Zakhem, MwanaFA amesema:
“Tulikuwa na wakati mzuri na ndugu zangu Ahmed Ally na Mwagala Christina pale Mbagala Zakhem jana kwenye hamasa ya CHAN 2024… Serikali imefanya sehemu yake kwenye upande wa maandalizi ya mashindano haya kama waandaaji na pia kama washiriki, na mahali palipobaki ni pa timu ‘kukiwasha’ na Watanzania wote kuiunga mkono na kufurahia mashindano haya sasa. Mungu ibariki Tanzania,”alisema.
Michuano ya CHAN 2024, inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee, inatarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu na kuwa jukwaa muhimu kwa vipaji vya ndani kuonesha uwezo wao na kuipeperusha vema bendera ya Taifa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi waandaaji wa mashindano hayo na juhudi mbalimbali za kiserikali zimeelekezwa katika kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa kiwango cha kimataifa. Nchi nyingine ni Kenya na Uganda.
MwanaFA amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuimarisha maendeleo ya michezo nchini, lakini akasisitiza umuhimu wa Watanzania kushiriki kwa moyo mmoja katika kuiunga mkono timu yao na kusherehekea mashindano hayo kwa amani na mshikamano.