
DAR ES SALAAM: STAA wa Simba, Joshua Mutale amerejesha tena tabasamu usoni kwake na kwa mashabiki wa Simba kwenye michezo aliyopata nafasi hivi karibuni.
Wakati anasajiliwa Simba matarajio yalikuwa makubwa kwake kabla ya mambo kwenda tofauti na mashabiki kumkataa wengine wakishinikiza afukuzwe kwenye dirisha dogo la usajili lililopita.
Siku za hivi karibuni nyota huyo wa Kimataifa wa Zambia ameanza kuwafurahisha mashabiki wa Simba, leo alikuwa kwenye kiwango bora dhidi ya Big Man FC kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB, mchezo ambao Simba imeshinda 2-1 na Mutale kuingia kambani.
Bao jingine la Simba limefungwa na Leonel Ateba kwa mkwaju wa penati huku Mussa Henock akifunga lakufuta machozi kwa Big Man.
Baada ya kumalizana na Big Man mnyama anatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry utakaopigwa Aprili 2.