Mr Blue: “Nilikutana na mke wangu club, Leo ndiye ninaishi naye

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Kheri Samee ‘Mr Blue’, amefichua namna alivyokutana na mke wake, Waheeda, akisema walifahamiana katika
mazingira ya starehe, jambo linaloonyesha kuwa mahali mtu anapokutana na mwenzake si lazima liamue hatima ya uhusiano wao.
Mr Blue ameyasema hayo kupitia Instagram Story yake, akieleza kuwa alikutana na Waheeda katika Klabu ya Bilicanas siku ya Jumapili mchana, wakati kulipokuwa na burudani ya ‘Disco Toto’.
“Ni kweli, mke wangu ninayeishi naye nilikutana naye Club Bilicanas, Jumapili mchana kulikuwa na Disco Toto,” amesema Mr Blue.
Amesema uhusiano wao ulianza mwaka 2003, kipindi ambacho alikuwa anaanza safari yake ya muziki na hatimaye msichana aliyekutana naye wakati huo ndiye aliyekuja kuwa mke wake.
“Nimeanza naye 2003 wakati naanza game, nikapata demu ambaye ndiye yule mke wangu,” amesema.
Mr Blue pia ameeleza kuwa simulizi ya namna alivyokutana na Waheeda imewahi kuakisiwa kupitia wimbo wake ‘Baki na Mimi’, akisema baadhi ya mistari katika wimbo huo inaelezea ukweli wa safari yao.
Kwa upande mwingine, Mr Blue ametoa ujumbe kwa jamii akisisitiza kuwa mazingira ambayo mtu anakutana na mwenza wake hayapaswi kutumiwa kumhukumu mtu au kutabiri maisha yake ya baadaye.
Amesema hatima ya mtu katika suala la mapenzi na ndoa inaweza kuwa tofauti na matarajio ya watu, kwani mazingira ya kukutana si lazima yawe kipimo cha maisha ya baadaye.
“Hatima ndio hupanga utakuwa na nani na wapi; mazingira si sababu,” ameandika Mr Blue.




