Mpanzu: Bado sijafikia ubora wangu
DAR ES SALAAM: NYOTA wa Simba, Elie Mpanzu amesema licha ya kuonesha kiwango bora kwasasa lakini bado yupo kwenye asilimia 70 tu ya ubora wake.
Mpanzu alijiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili na ameanza kucheza mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo ameonekana kufanya vizuri.
Akizungumza kuhusu kiwango chake, Mpanzu amesema anafurahia mchango wake ndani ya timu lakini bado hajaonesha ubora wake wote.
“Nafurahi kuona Simba inafanya vizuri na kuwa sehemu ya wachezaji wenye mchango ndani ya timu, bado sijafikia asilimia 100 ya ubora wangu, niko kwenye 70%, ninaimani nikiendelea kupata nafasi, nitafikia kiwango ninachokitaka,” amesema.
Aidha, Mpanzu amesema ana imani kuwa Simba itafanya vizuri kwenye michezo iliyosalia, kwani malengo yao ni kufanikisha kampeni ya kutwaa ubingwa.
Amezungumza pia sare waliyoipata dhidi ya Azam FC, akisema ilikuwa pigo kwao, lakini sasa wanajipanga kwa mchezo unaofuata dhidi ya Coastal Union.
“Sare dhidi ya Azam FC ilituumiza, lakini tunasonga mbele. Sasa tunajipanga kuhakikisha tunapata alama tatu dhidi ya Coastal Union,” alisema Mpanzu.
Simba itakuwa ugenini dhidi ya Coastal Union katika mchezo utakaochezwa Jumamosi, Machi Mosi, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.