Moto wa Dar Derby! Debora, Asia wapishana kijeshi

DAR ES SALAAM: MABONDIA wa kike Debora Mwenda na Asia Meshack wamechimba mkwara kila mmoja akitamba kumtoa mwenzake nusu kaputi kwenye pambano la Dar Derby linalopigwa kesho jijini Dar es Salaam.
Ilikuwa ni kwenye zoezi la kupima afya na uzito pale Leaders Club, lakini hali ilichafuka ghafla baada ya Debora kumtupia Asia kombora la maneno na kutaka kulianzisha jukwaani.
“Mnasema mimi ni mrembo siwezi kupigana, Siyo kwa sura, siyo kwa umbo. Ulingoni siyo pa kupendeza, ni pa kupigana. Na mimi niko fiti kwa kila kitu, ni jasiri na nimefanya mazoezi ya kutosha ,” alisema Debora huku mashabiki wakimshangilia.
Asia hakubaki kimya, alikuja na majibu ya moto kama kawa:
“Mimi si bondia wa maneno, ni wa mikono. Hapa siyo pa kukurupuka. Kesho nitakukalisha vizuri, uelewe mchezo si maneno – ni kupigana!”
Mashabiki waliokuwa eneo hilo walilipuka kwa kelele, wengine wakishabikia, wengine wakishika tama.
Pambano la Dar Derby litahusisha zaidi ya mabondia 15 kutoka pande mbalimbali za Dar es Salaam.
Mashabiki wameombwa kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia nani ataibuka kidedea kati ya “Msomi wa Ulingoni” Debora au “Muuaji Kimya” Asia.