Africa

Mosimane aifumua Misri mbele ya Ramaphosa

CAIRO: TIMU ya Afrika Kusini wameendeleza kiwango chao bora chini ya kocha Pitso Mosimane baada ya kuichapa Misri bao 1-0 kwenye Uwanja wa Cairo, jana Jumapili.

Bao pekee la Bafana Bafana lililofungwa na Puso Dithejane dakika ya 51 lilitosha kuipa ushindi timu hiyo katika mchezo huo wa kirafiki na kuendeleza rekodi yao ya ushindi wa tatu mfululizo chini ya kocha huyo.

Mechi mbili zilizopita, timu hiyo imezifunga Guinea mabao 2-1 na Eritrea mabao 5-0 katika mechi za kuwania AFCON 2027, ikiongoza Kundi D kwa pointi 6.

Aidha, ushindi huo dhidi ya Misri pia ulishuhudiwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa aliyekuwa uwanjani hapo na kushuhudia timu hiyo iliyojumuisha nyuso kadhaa mpya katika kikosi hicho kilichopambana kwa ujasiri.

Imeripotiwa kuwa Ramaphosa alifika kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha timu hiyo uwanjani hapo, ili kuwatakia heri wachezaji dakika chache kabla ya kuanza kwa mechi.

Rais Ramaphosa yuko nchini Misri, ambako alishiriki katika Mkutano wa 8 wa Uratibu wa Katikati ya Mwaka wa Umoja wa Afrika, na alitambulishwa kwa timu hiyo na Rais wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini (SAFA), Dkt. Danny Jordaan.

Bafana Bafana inatarajiwa kurejea Johannesburg, Afrika Kusini, leo Jumatatu baada ya kumaliza rariba yake ya mechi za kimataifa ikisubiri kuendeleza kampeni yake ya kufuzu AFCON Novemba 13, mwaka huu itakapovaana na Kenya.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button