Ligi Kuu

Miloud: Ushindi wa Coastal Union chachu ya Derby dhidi ya Azam FC

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga,Miloud Hamdi , amesema ushindi walioupata dhidi ya Coastal Union ni hatua muhimu kuelekea mchezo wao mkubwa ujao, Dar es Salaam Derby dhidi ya Azam FC.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara unatarajiwa kuchezwa alhamisi, Aprili 10, katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Miloud amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Coastal Union licha ya kupoteza nafasi nyingi, unawapa nguvu na morali kuelekea pambano hilo muhimu.

“Tumecheza vizuri, tulipata nafasi zaidi ya sita lakini tukapata bao moja. Hizo pointi tatu ni muhimu sana kuelekea mchezo dhidi ya Azam FC,” amesema.

Kocha huyo ameongeza kuwa anaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyobainika katika mchezo huo, huku akisisitiza umuhimu wa wachezaji wake kuwa makini zaidi katika kutumia nafasi wanazozipata.

“Napenda kuona mchezaji anakuwa hatari katika eneo la mpinzani, anatengeneza nafasi na anazitumia vizuri ili tuweze kupata mabao mengi zaidi,” ameongeza.

Kwa upande mwingine, Miloud alikiri kuwa mechi dhidi ya Azam FC haitakuwa rahisi kwani kila timu inahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Tutakuwa tayari, huu ni mchezo wa ushindani mkubwa na kila timu itahitaji matokeo,” amesema.

Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na morali ya ushindi, huku wakitambua kuwa matokeo dhidi ya Azam FC yanaweza kuwa na maana kubwa kwenye mbio zao za kuwania ubingwa msimu huu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button