Michuano ya taifa Cup kuanza leo

DODOMA: MICHUANO ya Taifa Cup 2025 ya mpira wa kikapu inaanza rasmi leo jioni katika viwanja vya Chinangali, Dodoma, huku mechi za ufunguzi zikiwa kati ya Kigoma dhidi ya Iringa na Mara dhidi ya Arusha.
Mashindano hayo yanayoratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) yametaja zawadi kwa washindi mbalimbali msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya TBF, zawadi hizo ni pamoja na Sh 400,000/= kwa kila timu inayoshiriki hatua ya makundi. Sh 600,000/= kwa timu zitakazofuzu hatua ya robo fainali.
Dau litapanda kwa kila hatua ambapo kwa timu zitakazoingia nusu fainali zitapata sh 800,000 huku mshindi wa pili akitarajiwa kuondoka na sh milioni 4. Bingwa wa michuano hiyo ataondoka n ash milioni 7.
Aidha, wachezaji binafsi nao hawajasahaulika. Mchezaji Bora wa Mashindano (MVP) atazawadiwa TSh 250,000/=, huku tuzo za Mfungaji Bora, Mlinzi Bora, Chipukizi Bora, na Kocha Bora kila mmoja akipata zawadi ya TSh 200,000/=.
Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa TBF Mary Arthur alisema “Tunaamini Taifa Cup mwaka huu itakuwa ya kipekee zaidi kwa sababu ya maandalizi, ushiriki mpana wa timu kutoka mikoa mbalimbali, na hamasa kubwa kutoka kwa wadhamini wetu,”
Kwa mujibu wa ratiba, mashindano hayo yatachezwa kwa mfumo wa makundi kabla ya kuingia hatua ya mtoano.
Mwisho