Mapinduzi CupNyumbani

Michezo ya Mapinduzi iangaliwe zaidi

IJUMAA Januari 13, 2023 ilikuwa hitimisho la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 kwa Singida Big Stars ya Singida kuumana na Mlandege ya Zanzibar kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar ambapo Mlandege imetwaa taji hilo.

Michuano hiyo imefikia hitimisho siku moja baada ya Kumbukumbu ya Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Michuano hii imekuwa ikifanyika kila mwaka kwa ajili ya kuenzi Mapinduzi hayo kwa kushirikisha timu mbalimbali kutoka Bara na Visiwani na wakati mwingine nje ya nchi kama safari hii ilivyoalikwa Aigle Noir ya Burundi.

Ingawa ni takribani misimu mitatu sasa imepita hakukuwa na timu shiriki za nje ya nchi, lakini ushiriki wao umekuwa na tija kubwa na kivutio cha michuano hii.

Hata hivyo, kidogo kumekuwa na kuyumba au kutochukuliwa kwa uzito mkubwa mashindano haya licha ya kuandaliwa na kusimamiwa na Serikali ya Zanzibar na hata zawadi ya bingwa ya msimu huu ya Sh milioni 23 imekuwa chagizo zuri la mashindano hayo.

Lakini bado kuna mianya ya kuifanya michuano hii ikawa mikubwa kwa kuzingatia timu shiriki, mantiki ya michuano yenyewe na utekaji wa hisia za mashabiki wengi wa soka nchini.

Mapinduzi pia imekuwa ikitajwa kuwa miongoni mwa kiunganishi kikubwa cha kuonekana kwa vipaji vya Wazanzibari na kuonekana Bara na kwingineko Afrika Mashariki. Mfano wa karibu ni kiungo gumzo kwa sasa, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyeingia kwenye mgogoro na klabu yake ya Yanga kwa masuala ya mkataba.

Kipaji chake kinajulikana na alianza kuwa gumzo kupitia michuano hii hii akiwa na kikosi cha JKU kabla ya kuonekana lulu ya taifa.

Mbali na vipaji vya kina Fei na mambo mengine yaliyotajwa huko juu lakini kama kutakuwa na uboreshwaji wa Kombe la Mapinduzi na muingiliano wenye faida ndani ya msimu kama ilivyo michuano mingine, michuano hii inaweza kuwa na tija kubwa kwa taifa zima kwenye nyanja mbalimbali.

Kwa sasa kombe hilo hushindaniwa kuanzia katikati ya Desemba na kumalizika Januari 13. Ni kipindi kifupi ambacho hupelekea ligi kusimama na akili zote kuhamia Zanzibar kabla ya
kurejea kwenye michuano mingine.

Pamoja na hayo, kuna uwezekano wa kuipanua michuano hii na kuunguruma tangu mwanzo wa msimu mpaka Januari 13 ikiwa ndani ya ratiba za ligi zote mbili za Bara na Visiwani huku ukiandaliwa utaratibu maalumu na rafiki kwa timu shiriki za nchi jirani kwa
msimu husika.

Mfano mashindano ya Bara ni Ligi Kuu na Kombe la FA na timu chache zinazoshiriki kila msimu mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa uchache wa michuano, bado kunaweza kufanyika kitu na kuipandisha michuano ya Mapinduzi kuwa yenye ushindani na ubora wa hali ya juu kwa kila timu kuvutiwa kushiriki kila msimu likishirikiana na lile la Zanzibar (ZFF) wanaweza kuwa na ratiba nzuri kuanzia mwanzo wa msimu mpaka katikati ya msimu inapomalizika michuano hii bila ya kusimamisha ligi yoyote na michuano kuchezwa kwa miezi kadhaa kwa msisimko mkubwa.

Kifupi, timu zinaweza kuachwa zikashiriki ligi na makombe mengine kisha kuendelea na Mapinduzi pia kwa kucheza mechi zao husika kwa mchujo mpaka hitimisho la fainali.

Kulingana na miundombinu ya Zanzibar ya usafiri wake wa maji kutumia muda mfupi kutoka Dar es Salaam inaweza isiwe kikwazo kikubwa kwa timu za Bara kwa maana ya kwenda na kurudi baada ya kumalizika kwa mechi yake ya Mapinduzi.

Kwa upande wa timu za nchi jirani bado jopo la timu ya masoko ya michuano hii inaweza kufanya kitu kwenye udhamini wa masuala ya usafiri, malazi na vitu vingine husika vya michuano hiyo ili kurahisisha ushiriki wa majirani.

Takribani miaka 17 sasa imepita tangu uwepo mfululizo wa michuano hii, nafikiri sasa ni muda mwafaka wakati soka linakuwa kwa kasi nchini, nasi pia kuipandisha thamani michuano yetu kwa kutafuta namna ya kufanya kwa faida ya mchezo wa soka nchini.

Mapinduzi inaweza kuwa mbadala wa michuano ya Kombe la Kagame ambayo imekuwa ikifanyika kwa kuyumba mno hivi karibuni tofauti na miaka ya nyuma.

Hakuna asiyetambua msisimko wa Kombe la Kagame linaloshirikisha timu nyingi mashuhuri za Afrika Mashariki lakini halisikiki tena kama ilivyokuwa awali, kwa nini isitumike fursa hiyo kuiweka Mapinduzi kwenye ubora huo na kuzidi kujitambulisha?

Inawezekana kukawa na ugumu kulingana na uzoefu au utendaji wa mamlaka tulizonazo za soka nchini lakini hakuna kinachoshindikana kama kweli kutasukwa mikakati ya kueleweka
kuiboresha michuano hii ambayo ni mikubwa lakini imepewa hadhi ya udogo.

Kukuzwa kwa michuano hii kiutaratibu na mwongozo kunaweza pia kutufanya tukashuhudia vipaji vipya kila baada ya wiki kadhaa tangu kuanza kwa msimu mpaka Januari na kuongeza thamani ya mahitaji wakati wa dirisha dogo la Januari kila msimu.

Na si kutegea mpaka ifike Januari ndipo tuone vijana wachache katika mechi chache kwa siku chache. Tusiishie hapo bado tuna nafasi ya kukua kwa kadri tunavyoweza.

Nazungumzia uonekanaji wa vipaji vipya si tu kwa timu za Zanzibar bali hata timu shiriki za Bara ambazo pia hutumia michuano hiyo kuchomeka wachezaji wa vikosi vyao vya vijana ambao wanaonesha kukua.

Kingine kwa kushirikisha timu za nchi jirani na Ligi Kuu tangu msimu uanze mpaka Januari kutaibua angalau chachu ya ushindani inayoonekana kukosekana kwa timu za Zanzibar kwa
msimu wote na kuzipa maandalizi mazuri ya kila msimu kwenye michuano ya klabu Afrika.

Fursa ni pana sana, kuna faida lukuki kuipanua michuano hii kuwa mikubwa zaidi ya hapa na pengine kuwa maarufu Afrika, kwanini isiwe maarufu kama tunahitaji iwe maarufu,
tupate faida na ikuze mpira wetu?

Michuano hii kwa jina lake na inakofanyika, ni kitu kingine cha kufikiria pia kuitangaza nchi kupitia sekta mbalimbali hata za utalii na mambo mengine.

Ni suala la kujipanga tu lakini Mapinduzi ikiwekewa mifumo na kubadilishwa kidogo muundo wa mechi zake, inaweza kuwa na tija na chanzo kingine cha maendeleo ya soka na faida nyingine lukuki.

Related Articles

Back to top button