Matola: tunaaandaa dozi ya kubwa mno

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Simba, Selemani Matola ameweka wazi kuwa hawatakuwa na huruma na mpinzani wao, Kilimanjaro Wonders katika mchezo wa kesho wa kombe la Shirikisho (FA). Simba itashuka dimba la KMC kusaka ushindi katika mchezo huo wa hatua ya 64 bora ya kombe la FA dhidi wa timu hiyo kutoka Kilimanjaro.
Matola amesema mchezo huo ni muhimu kupata ushindi na hawatawabeza kwa udogo wa wapinzani hao na kupanga kikosi kamili katika mchezo huo wa kesho.
“Tumejipanga vizuri, huu ni mchezo wa mtoano hutakiwi kufanya makosa, tunauzoefu na timu hizi za chini, kwetu ni kama fainali hatutakiwi kuingia kwa dharau hakutakuwa na mabadiliko makubwa ya wachezaji,” amesema.
Kocha huyo amesema wataingia kwa heshima na tahadhari kubwa kwa sababu wana kumbukumbu ya kuondolewa katika michuano hiyo na timu aina ya Kilimanjaro Wonders misimu iliyopita.
“Hutakiwi kupanga kikosi cha kawaida kwa mpinzani wetu, tunaweka ‘Full Dozen dhidi ya Kilimanjaro Wonders haijalishi uchanga wa timu hiyo,” amesema.
Kwa upande wa kocha wa Kilimanjaro Wonders, Daudi Macha amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri, wamekuja kwa lengo la kupambana dhidi ya Simba, wanacheza kulingana na mazoezi waliyoyafanya kabla ya mchezo.
“Tunaiheshimu Simba timu kubwa ukizingatia timu yetu ni changa, huu ni mchezo wa mpira wa miguu, kuna kujifunza na kupambana. Kisaikolojia tupo vizuri na vijana wetu wanajua wanaenda kukutana na timu gani, wameniambia mazoezini wanaenda kupambana kwenye mchezo wa kesho,” amesema.
Macha amesema wachezaji wanatambua huu mchezo ni sehemu ya kuonekana, sio wageni wa uwanja wala umati wa mashabiki uwanjani bali ni ugeni wa wachezaji wa Simba wanaocheza nao.