Serie A

Mashabiki wapinga mechi za ‘Serie A’ Australia

SYDNEY: KUNDI la mashabiki wa soka barani Ulaya, Football Supporters Europe (FSE), limeitaka Serie A ya Italia kufuata mfano wa La Liga ya Hispania na kuachana na mpango wa kupeleka mechi ya kawaida ya ligi kati ya AC Milan na Como katika jiji la Perth nchini Australia, mapema mwakani.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya La Liga kutangaza kuondoa pendekezo lake la klabu ya Villarreal kucheza dhidi ya Barcelona nchini Marekani, kufuatia upinzani mkali kutoka kwa wachezaji na mashabiki wa soka nchini Hispania.

“Huu ni ushindi mkubwa kwa soka la Ulaya na kwa kila mtu anayeamini kwamba mchezo huu ni sehemu ya jamii zetu. Sasa ni wakati wa Serie A pia kuachana na mpango wake”

“Serie A inapaswa kufanya uamuzi sahihi mbele ya upinzani unaoongezeka. Wachezaji na mashabiki nchini Italia wameshaweka msimamo wao wazi kabisa kuendelea na wazo hili lililoshindikana kutaiharibia ligi heshima yake, soka la Italia, na mchezo mzima kwa ujumla. Mchezo huo hauna sababu ya kuchezwa umbali wa kilomita 15,000 kutoka nyumbani kwake.” – FSE imesema kupitia taarifa yake iliyosambazwa jana Jumatano.

Hadi sasa, Serie A haijasema chochote huhku wadau wa soka wakisema ukimya wa viongozi wa ligi hiyo unaashiria kuwa hawana mpango wa kubatilisha uamuzi wao ambao unaonekana kuwa na faida kwa umaarufu wa ligi hiyo.

AC Milan tayari imepata kibali kutoka kwa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) kuruhusu mchezo huo wa Februari kuchezwa kwenye Uwanja wa Perth Stadium, kipindi ambacho uwanja wa San Siro hautapatikana kutokana na maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Milano-Cortina.

Hata hivyo, mchezo huo unahitaji idhini zaidi kutoka kwa Shirikisho la Soka la Australia (Football Australia), Shirikisho la Soka la Asia (AFC), na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kabla ya kuthibitishwa rasmi.

Wakati klabu nyingi kubwa za Ulaya huwa zinacheza michezo ya kirafiki kabla ya msimu katika miji mbalimbali duniani, mechi ya AC Milan dhidi ya Como itakuwa ya kwanza ya Serie A kuchezwa nje ya Italia.

Kiungo wa Mfaransa wa AC Milan, Adrien Rabiot, alinukuliwa mapema mwezi huu kwamba mpango huo ni “wa kipuuzi” na “hauingii akilini,” lakini kauli zake zilipuuzwa na Mtendaji Mkuu wa Serie A, Luigi De Siervo, aliyesema wachezaji wanapaswa “kuelewa thamani ya fedha wanazopata na kuheshimu waajiri wao.”

Related Articles

Back to top button