Maresca: Palmer ana shida binafsi

LONDON:KOCHA mkuu wa Chelsea Enzo Maresca amesema kushuka kiwango kwa Mshambuliaji wake Cole Palmer ni suala binafsi la kisaikolojia na si matatizo ya benchi la ufundi kama inavyotafsiriwa na wadau wengi wa soka.
Palmer mwenye miaka 22 alianza vizuri msimu wake wa kwanza na Chelsea akifunga mabao 27 na asisti 15 katika michezo 48 aliyovaa jezi ya bluu lakini msimu huu amefumania nyavu mara 14 pekee kwenye mashindano yote mpaka hivi sasa akiwa na ukame wa mechi 16 bila bao.
Maresca anasema bado ana Imani mchezaji huyo anaweza kurekebisha matatizo yake na kurejea kwenye ubora aliouonesha msimu uliopita kama mshambuliaji huyo ataondoa wasiwasi na kujisikia vibaya kwa kushindwa kuisaidia timu.
“Kwa hakika ni jambo la kisaikolojia, si la mbinu wala kiufundi, Cole bado ndiye yule mchezaji aliyefunga mabao 14 katika mechi 20. Mtindo ni uleule, meneja ni yule yule, klabu ni ile ile, hakuna kilichobadilika kwa Cole, ni saikoloji tu wakati huu”.
“Unaweza kuona ana wasiwasi kidogo kwa sababu anataka kuisaidia timu. Unaweza kuona wazi kuwa anajituma sanakwenye hilo. Lakini mliona jinsi alivyokuwa na furaha baada ya mechi na Fulham. Ni suala la muda tu kama tunaweza kushinda mechi. Hakika atafunga mabao”. – amesema Maresca
Chelsea wako nafasi ya sita kwenye msimamo wa Premier League wakiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 33, huku wakiwinda nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Wanawafuata Newcastle United walio katika nafasi ya tano kwa pointi mbili. Timu tano za Premier League zimehakikishiwa nafasi ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu wa 2025-26.