Man UTD yakubali dili la Onana

MASHETANI Wekundu, Manchester United imekubali dili la euro milioni 55 sawa na shilingi bilioni 123 kumsajili golikipa wa Inter Milan, Andre Onana.
Klabu hiyo yenye makao yake Old Trafford italipa ada ya pauni milioni 43.8 kwa ajili ya nyota huyo wa kimataifa wa Cameroon pamoja na nyingeza ya pauni milioni 3.4.
United ina tumaini Onana mwenye umri wa miaka 27 atajiunga na timu hiyo katika ziara ijayo Marekani lakini itapaswa kugharamia visa kwa ajili yake.
Kocha Erik ten Hag alianza mipango ya kumsajili golikipa huyo msimu uliopita na anahisi Onana anaweza kuwa usajili muhimu kwenye kikosi cha United na uamuzi wake umechochea David de Gea kukataa ofa ya mkataba mpya.
Onana alitumikia Ajax kwa miaka saba kabla ya kuhamia Inter Julai 2022.
Alicheza michezo 24 ya Serie A bila kufungwa goli Inter ikishaka nafasi ya tatu na pia hakufungwa goli katika michezo 13 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita akiwa golikipa bora kwenye michuano hiyo.
Golikipa huyo alicheza mechi ya fainali Ligi ya Mabingwa dhidi ya Manchester City mwezi uliopita Inter ilipopoteza kwa goli 1-0.
Onana anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa United majira haya ya joto baada ya kiungo Mason Mount akitokea Chelsea kwa ada ya awali ya pauni milioni 55.