Malkia wa Uswazi kumvaa Dorisia Desemba 26

DAR ES SALAAM: BONDIA Dorothea Mhoza maarufu kwa jina la Malkia wa Uswazi, kutoka Gongo la Mboto, amemtambia kumpiga mpinzani wake Dorisia Mazige wa Dodoma kuelekea pambano la Usiku wa Mabingwa litakalofanyika Desemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Dorothea amesema licha ya kutambua uwezo wa Dorisia, anaamini maandalizi anayofanya yatamwezesha kuonesha ubora wake na kuibuka na ushindi katika pambano hilo.
Akizungumza wakati akiendelea na maandalizi, bondia huyo amesema yuko tayari kukabiliana na changamoto ya mpinzani wake, akisisitiza kuwa anataka kutumia pambano hilo kuthibitisha uwezo wake ndani ya ulingo.
Kwa upande wake, Kocha wa Dorothea, Omary Zungu, amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha bondia wake anaingia ulingoni akiwa na mbinu na ufundi wa kutosha kumkabili Dorisia.
Zungu amesema maandalizi wanayofanya yanalenga kuhakikisha Dorothea anakuwa katika kiwango kizuri cha ushindani ili kuweza kupata matokeo wanayoyatarajia katika pambano hilo.




