Masumbwi

Mabondia waiomba Azam Media kuurudisha mchezo wa ngumi

DAR ES SALAAM:MABONDIA wa ngumi za kulipwa nchini wameiomba Azam Media irejee kuonesha mapambano ya ngumi, wakisema kusitishwa kwa matangazo hayo kuliwaweka kwenye wakati mgumu kiuchumi na kijamii.

Mabondia hao, wakiwemo Ibrahim Class, Mfaume Mfaume, Abdallah Pazi maarufu kama ‘Dulla Mbabe’, Nassibu Ramadhan na wengine, wamesema baada ya kesi kati ya bondia Amos Mwamakula na Azam kumalizika, wana matumaini kwamba Azam itarejea upya kuonesha mapambano ya ngumi.

“Tulipitia kipindi kigumu. Mimi binafsi nilikata tamaa hadi nikaacha kufanya mazoezi. Lakini sasa, baada ya Azam kushinda kesi, nimepata nguvu upya na nimerudi mazoezini,” alisema Mfaume Mfaume.

Kwa upande wake, Ibrahim Class amesema Azam TV iliwasaidia sana kujulikana na kupata mafanikio.
“Leo hii nina nyumba, nina gari, ni kwa sababu ya Azam. Walitutoa mbali sana. Tunaomba warudi kwa nguvu zote,” Amesema Class.

Nassibu Ramadhan naye alieleza namna maisha yao yalivyokuwa magumu baada ya Azam kusimamisha matangazo ya ngumi.
“Azam walitufanya tujulikane. Tumepitia maisha magumu, lakini sasa tuna matumaini upya. Bila Azam, hakuna kinachoendelea,” amesema Ramadhan.

Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ alishukuru uamuzi wa Mahakama na serikali kwa kufanikisha suala hilo.

“Tulilazimika kurudi kwenye kazi zetu za zamani ili kuishi. Kiukweli tulikumbwa na njaa. Tunaomba Azam warudi, tuanze tena mapambano, hata tukianzia sisi kwa sisi,” amesema Dulla Mbabe.

Bondia chipukizi Rahim Omar amesema vijana wengi walikuwa wamekata tamaa kwa kuwa Azam ilionekana kuwa njia yao ya mafanikio.

“Tuliona matumaini makubwa kupitia Azam. Tunawaomba warudi, tuendelee kuonesha vipaji vyetu,” alisema.

Mabondia hao walisema mapambano ya ngumi yakirejea kupitia Azam, si wao tu watakaonufaika bali pia vijana wengi wanaochipukia, familia zao na mashabiki wa mchezo huo kote nchini.

Related Articles

Back to top button