Ligi ya Taifa ya Kikapu kuchezwa Novemba 26

DAR ES SALAAM: LIGI ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL) hatua ya mchujo inatarajiwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Novemba 26 hadi Desemba 6, 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kutafuta wawakilishi wa Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa mwakani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), ligi hiyo itahusisha jumla ya timu 16 za wanaume, zikiwemo timu nne zilizofika hatua ya nusu fainali msimu uliopita; Dar City (Dar es Salaam), ABC (Dar es Salaam), UDSM Outsiders (Dar es Salaam) na Kisasa Heroes (Dodoma), pamoja na timu nyingine 12 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa wanawake, jumla ya timu 12 zitashiriki, zikiungana na timu nne zilizotamba msimu wa 2024 ambazo ni Fox Divas kutoka Mara, DB Lioness, JKT Stars na Vijana Queens zote za Dar es Salaam.
TBF imesema ligi hiyo ni muhimu kwa sababu itatoa mwanga wa ni timu zipi zitaiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Basketball Africa League (BAL) kwa upande wa wanaume, Africa Women Basketball League (AWBL) kwa upande wa wanawake pamoja na East Africa Champions Cup (EACC).
“Tunatarajia ushindani mkubwa, tunazikaribisha timu zote kufanya maandalizi ya kutosha ili kuonesha ubora wa mchezo na kuitangaza vema nchi yetu kimataifa,” imesema TBF kupitia taarifa yake.
Aidha, dirisha la usajili wa wachezaji litafunguliwa Novemba 8 na kufungwa Novemba 18, 2025 ili kuruhusu taratibu za maandalizi kuendelea kwa wakati.
Viongozi wa vyama vya mikoa wametakiwa kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa timu zao kuhusu ratiba na utaratibu wa usajili.
TBF pia imetoa angalizo kwamba kila mchezaji wa kigeni atapaswa kuwasilisha nakala ya pasipoti, barua ya uhamisho na uthibitisho wa uhamisho wa kimataifa ili kuthibitishwa kushiriki ligi hiyo.




