Africa

Karia aonya wanaoharibu soka Bongo

DAR ES SALAAM: RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amewataka wale wanaotaka kuharibu maendeleo ya soka nchini kuelekeza nguvu zao kwingine.

Akizungumza alfajiri alipowasili nchini akitokea Misri, Karia, aliyeshinda nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), alisema maendeleo ya soka la Tanzania yanaonekana, na baadhi ya watu wanataka kuliporomosha.

“Niwaambie kwenye mpira wetu wa Tanzania, sisi Shirikisho tupo makini. Kama kuna mtu hayupo makini ameona ana michezo yake, apeleke kwingine na si katika mpira wetu,” amesema Karia.

Aidha, amewashukuru Watanzania wote waliomuunga mkono katika mchakato huo na kusisitiza kuwa kazi ndiyo inayofuata badala ya kusherehekea.

“Tumepata nafasi hii, tusisherehekee sana, twende kufanya kazi. Mpira wetu ulipofika unaenda mbele zaidi. Nitakuwa katika vikao vya juu vya maamuzi ya soka Afrika, tofauti na awali nilipoingia kama mwalikwa kwa sababu ya urais wa CECAFA,” amesema.

Kuhusu nafasi yake ya urais wa CECAFA, Karia amesema  anatarajia kuiachia ili wengine waendeleze soka katika ukanda huo baada ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa CAF.

Related Articles

Back to top button