Kocha wa Tanzania Prisons apambana kuepuka kushuka daraja
DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Amani Josiah, ameanza kupigia hesabu alama 18 katika michezo sita iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuhakikisha timu yake inajiweka salama na kujiondoa kwenye presha ya kushuka daraja.
Tanzania Prisons kwa sasa inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi, ikiwa na alama 18 pekee, hali inayoiweka katika hatari ya kushuka daraja.
Ili kujinusuru, Josiah anasisitiza kuwa timu yake inapaswa kujipanga vizuri, hasa katika mechi zilizosalia, kuhakikisha inapata matokeo chanya.
Katika ratiba yao, Tanzania Prisons itacheza mechi nne za nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, JKT Tanzania, Coastal Union, na Yanga SC, huku ikicheza ugenini dhidi ya KenGold FC na Singida Black Stars.
Kocha huyo amesisitiza umuhimu wa kushinda michezo ya nyumbani ili kuhakikisha wanajiongezea nafasi ya kubaki kwenye ligi.
“Tunajua hali tuliyonayo si nzuri, lakini bado tuna nafasi ya kupambana. Tunahitaji kuhakikisha tunashinda mechi za nyumbani na kujaribu kupata matokeo mazuri ugenini,” amesema Josiah.
Baada ya kupoteza mchezo wao wa hivi karibuni dhidi ya KMC FC ugenini, Josiah amesema wamerudi kujipanga kwa ajili ya michezo ijayo, akisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia ili wasicheze kwa presha kubwa kutokana na nafasi mbaya waliyonayo.
“Tunafanya kazi kubwa kuhakikisha wachezaji wanakuwa na utulivu wa kisaikolojia. Hatutaki waingie uwanjani kwa presha, tunataka wajiamini na kucheza kwa bidii ili kufanikisha malengo yetu,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Josiah, mechi sita zijazo ni kama fainali kwao, na anawahimiza wachezaji wake kupambana ili kuhakikisha Tanzania Prisons inasalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.