Burudani

Kisa wajumbe Steve Nyerere asusia ubunge

DAR ES SALAAM: Msanii wa filamu nchini, Steve Nyerere, ametangaza kuwa hana mpango wa kugombea ubunge katika uchaguzi ujao, baada ya kukatishwa tamaa na matokeo ya zoezi la kura za maoni alilolishiriki hivi karibuni.

Akizungumza kwa hisia mseto, Steve Nyerere amesema alipata kura sita pekee kutoka kwa wajumbe, hali iliyomfanya aone wazi kuwa si muda wake wa kisiasa. Kwa kejeli na ucheshi wake wa kawaida, Steve aliweka wazi kuwa tayari ameshaomba rasmi kurudi kazini kwa bosi wake, Majizzo.

“Baada ya kupata kura sita kutoka kwa wabunge, nimeamua kurudi kazini. Nimewasiliana na bosi wangu Majizzo, nimemwambia nipo tayari kuendelea na kazi rasmi. Siasa si kila mtu kaka,” amesema Steve kwa mtazamo wa utulivu.

Steve, ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa katika tasnia ya filamu na mitandao ya kijamii, pia amekuwa mstari wa mbele katika harakati za kijamii kupitia taasisi yake inayohamasisha mawasiliano kati ya wazazi na watoto. Hata hivyo, hatua yake ya kutaka kujitosa kwenye siasa haikuungwa mkono kwa kiwango alichotarajia.

Kauli yake imeibua mijadala miongoni mwa mashabiki na wanaharakati wa sanaa na siasa, wengi wakitafsiri matokeo hayo kama ujumbe wa wazi kuwa si kila umaarufu kwenye sanaa unaweza kutafsiriwa kama tiketi ya mafanikio kisiasa.

Kwa sasa, Steve Nyerere anarejea katika kazi zake za kijamii na burudani huku akiendelea kutoa mchango wake kwa jamii kupitia vipindi, matukio ya sanaa, na kampeni za kijamii. Wito wake kwa wengine wanaotamani siasa: “Jiandae si kwa fomu tu, bali kwa ukweli wa kisiasa.”

Related Articles

Back to top button