Kisa kipigo, Arteta alia na mipira Carabao Cup

LONDON:Meneja wa Washika mitutu wa jiji la London Arsenal Mikel Arteta amesema wangeweza kuibuka na ushindi dhidi ya Newcastle United hapo jana kwenye Kombe la Carabao kama si ‘mipira isiyoaminika’ inayotumika katika mashindano hayo.
Arsenal walipiga jumla ya mashuti 23 katika mchezo huo lakini matatu pekee yalilenga lango yakiwemo lile la Gabriel Martinelli lililopiga nguzo, na nafasi ya wazi ya iliyokoswa ya Kai Haverts. Alipoulizwa kuhusu kutotumika huko kwa nafasi Arteta alisema hana cha kubadilisha katika kikosi na akagusia mpira unaotumika kwenye mashindano hayo.
“Tulipaisha mipira mingi juu ya lango, lakini ni ajabu mipira hii inavyopaa kwa kasi ya kushangaza hivyo naona tuna kazi ya kufanya. Naona ni tofauti tuu, tofauti yake ni kubwa sana na mpira wa ligi kuu ambao tumeuzoea na kuutumia muda mwingi tunapaswa kuzoea hili hata ukiugusa unajua ni tofauti” – Amesema Arteta
Mpira unaotumika katika Carabao Cup umetengenezwa na kampuni ya Puma wakati ule wa Ligi kuu ya England umetengenezwa na kampuni ya Adidas na kabla ya kipigo cha 2-0 dhidi ya Newcastle Arsenal wamefunga magoli 11 katika mechi tatu za kombe hilo msimu huu.