
KITENDO cha Azam kufungwa na Yanga mara kwa mara katika Ligi Kuu Tanzania Bara kimemkera nahodha wa timu hiyo Bruce Kangwa na amewataka wachezaji wenzake kujitathimini.
Akizungumza na SpotiLeo Kangwa amesema kinachomuuma ni kuona Yanga ndio timu pekee kwenye ligi inayokatisha ndoto za ubingwa za klabu hiyo katika misimu mitatu mfululizo ya karibuni.
“Tunapaswa kujitathimini kwa nini tufungwe na timu moja Kila msimu tena tukiwa nyumbani na Yanga ndio inayofifisha malengo yetu ya ubingwa ipo haja ya kuliangalia hilo,” amesema Kangwa.
Nahodha huyo amesema ameliomba benchi la ufundi na uongozi kulifanyia kazi kwa undani suala hilo ili kujua wapinzani wanawazidi wapi mpaka wanashindwa kupata ushindi.
Azam ilipoteza mechi zote mbili kwenye ligi msimu uliopita huku msimu huu Yanga ikichukua pointi nne kwa Azam baada ya kutoka sare mchezo wa kwanza na kufungwa mabao 3-2 katika mchezo wa marudiano uliochezwa Desemba 25.