
LONDON:NAHODHA wa timu ya taifa ya England, Harry Kane, anaamini anaweza kuwa mchezaji aliyekitumikia kikosi cha Three Lions mara nyingi zaidi atakapostaafu, huku akilenga kulitwaa Kombe la Dunia la 2026 litakalofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Kane, mwenye umri wa miaka 31, alicheza mchezo wake wa 105 Jumatatu katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Latvia, ambapo alifunga bao lake la 71 kwa timu ya taifa katika dakika ya 68.
“Hilo linawezekana, na nimesema mara kadhaa kuwa nataka kuitumikia England kwa muda mrefu niwezavyo. Najua kuna michezo mingi kuelekea Kombe la Dunia, halafu kuna mechi 10 kwenye michuano yenyewe,” alisema Kane.
“Wiki hii nimetimiza miaka 10 tangu nilipoichezea timu ya taifa kwa mara ya kwanza. Imekuwa safari nzuri yenye changamoto na mafanikio mengi. Sasa ni zama mpya na ukurasa mpya, ninafurahi sana na nataka kuendelea kwa miaka mingi zaidi ili kuisaidia timu hii kufika mbali. Sisi, kama wachezaji na mashabiki, tunataka kushinda kombe kubwa,” aliongeza.
Kwa sasa, Kane yuko nyuma ya kipa wa zamani wa England, Peter Shilton, kwa michezo 20. Shilton ndiye anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi kwa timu ya taifa ya England. Kane pia anashindana na majina makubwa kama David Beckham, Frank Lampard, Wayne Rooney na wengine wengi kwenye orodha ya wachezaji waliovaa jezi ya England mara nyingi zaidi.