Justin Bieber alipwa dola milioni 10 kutumbuiza kwa Bilionea Ambani
MUMBAI: MWANAMUZIKI Justin Bieber ameripotiwa kulipwa dola milioni 10 za kimarekani kutumbuiza kwenye sherehe kabla ya harusi ya mrithi wa bilionea Anant Ambani huko Mumbai nchini India.
Mwimbaji huyo mwenye miaka 30, anadaiwa kupata pesa nyingi zaidi kwa ajili ya kuimba nyimbo zake zaidi ya kumi zikiwemo ‘Love Yourself’ na ‘Peaches’ wakati wa tamasha la faragha la Anant, mchumba wa mfanyabiashara huyo Radhika Merchant, familia yao pamoja na marafiki zao.
Justin ana wastani wa utajiri wa dola milioni 300 amechapisha mfululizo wa picha na video za tamasha hilo kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa pamoja na bibi na bwana harusi watarajiwa.
Justin pia alishiriki picha zake akiwa India akifurahia safari ya gari la abiria hadi ukumbini kwa tafrija yake binafsi ambayo ilijaa wageni wengi huku akionyesha chumba cha hoteli aliyofika katika eneo hilo la Mumbai.
Mara tu baada ya onyesho lake, Justin alirudi Marekani na kujumuika na mpenzi wake mwanamitindo Hailey Bieber mwenye miaka 27, ambaye ni ujauzito na wanataraji kupata Watoto wa kwanza.
Mrithi wa India Anant ni mtoto wa mwenyekiti na mkurugenzi mkuu wa Reliance Industries Mukesh Ambani, ambaye ndiye mtu tajiri zaidi barani Asia na anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 123.4.
Harusi ya familia hiyo Tajiri inatarajiwa kufanyika Julai 12 mwaka huu. Mwezi Machi Rihanna mwenye miaka 36, aliripotiwa kulipwa dola milioni 6 ili kuwatumbuiza wanandoa hao kwenye sherehe iliyohudhuriwa na mabilionea wenzake akiwemo Bill Gates na Mark Zuckerberg.
Mnamo Mei, familia ya Anant ilialika jamaa kwenye safari ya siku tatu kutoka Italia hadi Ufaransa ambayo iliangazia maonyesho ya wanamuziki Katy Perry mwenye miaka 39, Pitbull mwenye miaka 43 na David Guetta mwenye miaka 56.