Johny Depp aweka wazi kurejea katika filamu ya Pirates of the Caribbean 6

HOLLYWOOD: MUIGIZAJI maarufu Johnny Depp ameonesha nia ya kurejea katika nafasi ya Kapteni Jack Sparrow kwenye filamu mpya ya Pirates of the Caribbean 6.
Depp amesema yuko tayari kurejea iwapo filamu hiyo itaandaliwa kwa namna inayoweza kuhitimisha vyema safari ya mfululizo huo.
Katika mahojiano na kituo cha Entertainment Tonight, Depp alisema anatamani kushiriki ili kuipa historia ya filamu hizo hitimisho zuri zaidi.
Pia ameeleza kuwa yuko tayari kufanya kazi na mtayarishaji Jerry Bruckheimer wakati wowote, akitaja urafiki wao wa muda mrefu.
Awali, Bruckheimer alithibitisha kuwa mazungumzo na Depp yanaendelea huku maandalizi ya muswada wa filamu mpya yakiendelea.
Depp ameigiza Kapteni Jack Sparrow katika filamu tano za mfululizo huo, kuanzia The Curse of the Black Pearl mwaka 2003 hadi Dead Men Tell No Tales mwaka 2017.
Mfululizo wa Pirates of the Caribbean umeingiza zaidi ya dola bilioni 4.5 duniani kote, huku mashabiki wakisubiri kuona iwapo Depp atarejea tena katika nafasi iliyompatia umaarufu mkubwa.




