Kwingineko

“Japan inaweza kushinda kombe la Dunia” – Honda

HONG KONG: mmoja wa mastaa wakubwa wa soka nchini Japan Keisuke Honda amesema Timu ya Taifa hilo inao ubora na kiwango cha juu hivyo ina uwezo wa kushinda Kombe la Dunia la mwakani nchini Marekani, Canada na Mexico.

Honda ambaye alicheza mechi 90 na timu ya taifa ya Japan na kushiriki Kombe la Dunia mara tatu, ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Shirika la Habari la Reuters wakati wa mkutano wa AVCJ Private Equity Forum mjini Hong Kong.

“Wana uwezo wa kufika angalau hatua ya nne bora kwenye Kombe la Dunia mwakani, labda hata kuwa mabingwa Hakuna lisilowezekana, na wana wachezaji wengi wazuri sasa, kwa hiyo natumai watatoboa,” amesema Honda.

Japan tayari imefuzu kwa Kombe la Dunia la mwakani litakalofanyika Amerika Kaskazini. Katika makala iliyopita nchini Qatar mwaka 2022, waliwafunga vigogo wa Ulaya Hispania na Ujerumani katika safari yao ya kufika hatua ya 16 bora.

Honda, mwenye umri wa miaka 39, alicheza soka katika nchi takriban tano, ikiwemo Italia katika klabu maarufu ya Serie A, AC Milan. Sasa akiwa mwekezaji wa kampuni za kuanzisha biashara (startups) nchini Japan na Marekani, Honda aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa bado hajakata tamaa na ndoto yake ya soka.

“Ndoto zangu sasa ni mbili kuwa mwekezaji bora duniani na kuwa kocha bora duniani, ambayo inamaanisha kushinda Kombe la Dunia kama kocha,” amesema.

Kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali aliambia Reuters pembezoni mwa mkutano huo kwamba anatumai siku moja kuwa kocha wa timu ya taifa ya Japan.

Kampuni yake uwekezaji imekusanya takriban yen bilioni 15.3 katika mfuko wake wa kwanza wa uwekezaji Januari, ikiwa na uungwaji mkono kutoka taasisi kama Sumitomo Mitsui Banking Corporation, SBI Group na Nomura, kwa mujibu wa taarifa ya X&KSK wakati huo.

Honda pia ni mwanzilishi mwenza wa Dreamers VC pamoja na muigizaji wa Kimarekani Will Smith. Taarifa kwenye tovuti yake zinaonesha kuwa kampuni hiyo inawekeza kwenye sekta za matumizi, teknolojia, burudani na bioteknolojia nchini Marekani.

Related Articles

Back to top button