FIFA yahaha kujaza viwanja Marekani

MIAMI: Shirikisho la soka Duniani FIFA linapambana kuona uwezekano wa kujaza Uwanja katika mchezo wa ufunguzi wa kombe la Dunia la Klabu kati ya Inter Miami ya marekani na Al Ahly FC ya Egypt baada ya muitikio wa mashabiki kununua tiketi za mchezo huo kuwa mdogo.
Uwanja wa Ufunguzi wa Kombe la Dunia la Klabu wa Hard Rock unabeba mashabiki 65,000 lakini kufikia asubuhi ya leo Alhamisi tiketi zilizouzwa ni tiketi 20,000 pekee jambo ambalo FIFA hawakulitarajia kwenye mchezo wa Ufunguzi ambao unahusisha Klabu enyeji ya mji huo.
Kwa mujibu wa Jarida la The Athletic, FIFA imefanya mbinu mpya ya kuujaza Uwanja huo kwa kushusha bei ya tiketi za mchezo huo kutoka dola 230 (shilingi laki 594,550) hadi dola 55 (kati ya laki 142,000 na149,000)
Sambamba na hilo taarifa zaidi kutoka Marekani zinasema FIFA imeingia Ubia na Chuo Kikuu cha Miami Dade chenye zaidi ya Wanafunzi 100,000 na kutoa ofa kwa kila Mwanafunzi atakayenunua Tiketi atapewa tiketi 4 za ziada za kutazama michezo minne Bure huku Bei ya Tiketi moja ya ofa ikishuka mpaka wastani wa shilingi elfu 10,391 za Kitanzania.
Soka si mchezo unaopendwa sana na watu wa Marekani tafiti mbalimbali zimeuweka mchezo huo katika nafasi ya 5 nyuma ya michezo maarifu zaidi kama American Football (NFL) unaoongozwa kwa watazamaji hasa fainali yake maarufu kama Super Bowl kisha kufuatiwa na michezo kama Basketball (NBA), Baseball (MLB), na Ice Hockey (NHL).