EPL haiishi mpaka iishe!

ENGLAND: Huenda umesikia mengi kuhusu ligi kuu nchini England maarufu sana duniani kote kwa chapa yake ya Premier League na ushindani wake usiotabirika hata watu kuipa jina la ligi ya kambare yaani haina mdogo kila timu ni kubwa.
Mengi yakushangaza yametokea katika ligi hii mengine labda umeyazoea kila kukicha, si ajabu aliyeshinda 5-0 leo akakandwa 7 wiki ijayo. Maajabu mengine ni usukani wa ligi ambao si kila aliyeushikilia mda mrefu alitwaa taji hilo mwisho wa msimu. Ili uamini ligi hii haiiishi mpaka iishe tunakuletea timu zilizowahi kuachwa kwa gepu kubwa la pointi kisha kutwaa ubingwa mwisho wa msimu.
Msimu wa 1997/98 Arsenal ilitwaa ubingwa wa ligi hiyo licha ya kuwa nyuma ya vinara wa ligi msimu huo Manchester United kwa pointi 13 kufikia mwezi Disemba mwaka 1997.
Manchester United walishafanya hivyo mara 5 katika historia ya ligi hiyo wakianza katika msimu wa 1992/93 walipotwaa ubingwa kipindi hicho ikiitwa Carling Premiership wakiwa nyuma ya Norwich city kwa pointi 12 kufikia mwezi Desemba 1992. Kisha Msimu wa 1995/96 wakiwa pointi 12 nyuma ya Newcastle kufikia Januari 1996.
Man United walirudia unyama huo walipotwaa ubingwa msimu wa 1996/97 baada ya kuwa nyuma ya majogoo Liverpool kwa pointi 10 kufikia Desemba 1996. Kisha kuwafanyia tena washika mitutu wa jiji la London Arsenal msimu wa 2002/2003 kwa pointi hizo hizo 10 kufikia Novemba 2002 kabla ya kuwarudia Liverpool kwa pointi 10 tena mwaka 2008 katika msimu wa 2008/2009.
Manchester City ndio kumbukumbu ya hivi karibuni, tukirejea msimu wa 2018/19 walipotoka nyuma kwa pointi 10 dhidi ya Liverpool kufikia Desemba mwaka 2018 na kutwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi moja pekee na kuwa klabu ya kwanza kushinda makombe matatu ya ndani (Domestic Treble)
Msimu huu Liverpool wanaongoza msimamo wa ligi kuu nchini England kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya Arsenal walio nafasi ya pili, vipi mdau unaona dalili za meza kupinduka?