“Duma” kuja na Tamthilia mpya Time of Love

DAR ES SALAAM: MSANII na mtayarishaji wa filamu nchini, Daudi Michael Tairo (Duma), anatarajia kuja na tamthilia mpya iitwayo Time of Love, itakayorushwa kupitia YouTube Channel yake ya Duma TV.
Akizungumza na Spoti Leo, Duma amesema wazo la kutengeneza tamthilia hiyo limekuja baada ya mafanikio aliyoyapata kupitia kazi zake zilizopita, ikiwemo Fundi na nyinginezo.
“Tumejipanga kutoa kazi bora zaidi kupitia Time of Love, ambayo itaguswa na maisha halisi ya watu, upendo, na changamoto za kijamii,” amesema Duma.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga, amemtembelea Duma ofisini kwake kujionea maendeleo ya kazi zake za utayarishaji wa filamu.
Akiwa katika ziara hiyo, Dk Kasiga amepata fursa ya kutazama maandalizi ya tamthilia hiyo mpya na kupongeza jitihada zinazofanywa na timu nzima ya Duma TV.
“Nawapongeza Duma na wenzake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Bodi ya Filamu itaendelea kushirikiana nao na wadau wengine katika kuhakikisha sekta hii inakua na kutoa ajira kwa vijana,” amesema Dk Kasiga.
Aidha, Dk Kasiga amesifu programu maalumu iliyoanzishwa na Duma kwa ajili ya kukuza vipaji vipya, akisema imekuwa chachu kubwa katika kugundua na kuendeleza uwezo wa wasanii chipukizi nchini.
Bodi ya Filamu Tanzania imeweka utaratibu wa kutembelea maeneo ya utayarishaji wa filamu ili kubaini changamoto wanazokabiliana nazo watengenezaji na kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya sekta ya filamu nchini.




