Dortmund yamnasa fundi kutoka EPL

Klabu ya Borussia Dortmund imetangaza kumsajili kiungo wa Ujerumani, Pascal Gross kutoka timu ya Brighton and Hove Albion kwa mkataba wa miaka miwili.
Taarifa zinaeleza kwamba Dortmund imelipa ada ya Euro milioni 10 pamoja na bonasi kupata saini ya mchezaji huyo mwenye miaka 33.
Gross anajiunga na klabu hiyo baada ya kuhudumu Brighton kwa miaka 7 ambayo alijiunga nayo akitokea FC Ingolstadt mwaka 2017.
Gross ameichezea Brighton michezo 228 ya Ligi kuu England na kufunga mabao 30 huku akitoa pasi zilizozalisha mabao 45 na kuisaidia Brighton kufuzu kucheza katika kombe la Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao ya miaka 122 baada ya kumaliza nafasi ya 6 kwenye msimu wa 2022-23.
Mchezaji huyo amewahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa klabu kwa nyakati mbili, katika msimu wa kwanza akiwa na klabu hiyo, na msimu uliopita ambao ndio ulikuwa wa mwisho kwake.
Dortmund wamemsajili Gross baada ya kuwa na msimu mbaya wa ndani. Licha ya kufanikiwa kufika hatua ya fainali ya Mabingwa Ulaya, ambapo walipoteza dhidi ya Real Madrid, pia walishika nafasi ya 6 katika msimamo wa Bundesliga na walitoka katika hatua ya 16 ya kombe la Ujerumani.